Göttinger Predigten

Choose your language:
deutsch English español
português dansk

Startseite

Aktuelle Predigten

Archiv

Besondere Gelegenheiten

Suche

Links

Konzeption

Unsere Autoren weltweit

Kontakt
ISSN 2195-3171





Göttinger Predigten im Internet hg. von U. Nembach

Easter Sunday, 08.04.2007

Predigt zu Mark 16:1-8, verfasst von Dawson E. Chao

SIKU YA KUKUMBUKA UFUFUO WAKE YESU KRISTO (PASAKA)

NENO KUU: "YESU KRISTO AMEFUFUKA HALELUYA"

Neno: Mk. 16: 1- 8

Kusudi: Wote wapate kuamini ufufuo wa Yesu Kristo, waone tumaini la uzima wa milele ndani yake Kristo, ambaye ndiye njia kweli na uzima.  Wajitoe kumtumikia kwa uaminifu wakieneza Injili (Habari Njema) ya ukombozi uliopatikana kwetu katika kifo na ufufuko wa Yesu Kristo. (Yn. 11:25 - 26); (I Kor. 15:20,21)

Wazo la Siku: Kwa nini mnamtafuta Aliye hai katika wafu? Hayupo hapa, Amefufuka kweli kweli (Lk. 24:5 -6).  Yesu yu hai ni mzima haleluya. Nendeni mkawaambie wanafunzi, pamoja na Petro, Awatangulia kwenda Galilaya, huko ndiko mtamwona.

 

I.  Utangulizi:

Leo ni sikukuu ya Pasaka I, siku ambayo wakristo kote ulimwenguni tunakumbuka kwa kusherekea kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo.  Sote tunashangilia kwa furaha tukisema, "Yesu Kristo Amefufuka!  Itikio: Amefufuka kweli kweli, Haleluya!  Hii ndio salamu ya Pasaka leo.

Wainjilisti  wote wanne (4) yaani: Mathayo, Marko, Luka na Yohana, wameshuhudia habari hii ya Ufufuo wa Yesu Kristo; kila mmoja kwa namna yake. Habari hii ya Ufufuo ni muhimu sana katika imani yetu sisi Wakristo (Ikor. 15: 3 - 4, 12 - 17, 20ff)  " Lakini sasa Kristo amefufuka katika wafu, limbuko lao waliolala."

 

II.  Habari Njema za Ufufuo wa Yesu Kristo Tumaini Letu

Katika somo la leo tunasoma kwamba, ni siku ya kwanza ya juma yaani Jumapili kama leo, baada ya Sabato, alfajiri mapema, kulipopambazuka  ndipo wamama mashujaa waliompnda Yesu, waliomtumikia Yesu, wanafunzi wasio rasmi walichukua hatua kuelekea kaburini, ili yamkini kukamilisha mambo muhimu ya maziko.

Wanawake hao ni Mariamu Magdalena, Mariamu wa Yakoo na Salome.  Hao walijiandaa vizuri, walinunua manukato na kuwa tayari kwenda kuupaka mwili wa Yesu kule kaburini (Lk. 24: 1 - 12)

Kwa nini?

(a)    Walitaka kuhakiki kama mwili wa Yesu umehifadhiwa vizuri (maziko), ikizingatiwa kuwa ndio waliokuwa karibu naye, wakimtumikia mara nyingi kwa upendo na shukrani kwa yale mema aliyowatendea Mt. 16:9.

(b)    Maziko yake Yesu yalifanyika katika mazingira ya haraka haraka, siku ile ya Ijumaa (Kuu) hasa kwa vile Sabato ilikuwa inaanza muda si mrefu baada ya kifo cha Yesu msalabani.  Ni wakati wa maandalio ya Sabato, uliohimiza kutoa mwili msalabani na kuharakisha maziko, yamkini bila wao kutoa heshima zao za mwisho (Mk. 15: 40 - 41).

(c)    Pamoja na hayo yote, hao wanawake jasiri kama wanavyoonekana, walisahau jambo moja la msingi; walisahamu kwamba Yesu alikwishasema  kuwa atafufuka siku ya tatu baada ya kifo chake msalabani. Huu ndio udhaifu wao wale wanawake.

Laiti wangelikumbuka Ahadi ya Yesu kwa wanafunzi wake na kwa taifa lake, Israel kuhusu ufufuo.  Ingewapunguzia mahangaiko na uchovu mwingi, nao wangengojea kwa utulivu mwaliko wa kuungana naye tena kule Galilaya. (Mk. 16:7); (Mk. 14:28)

Ukweli ni kwamba katika maisha yetu Wakristo, pale tunaposita au kutetereka  au kuyumba katika Imani ndipo tunapata shida zisizokuwa za lazima kama tunavyoona hata hapa chini (Mk. 16:16: 3,8) "Ni nani atakayetuviringishia lile jiwe mlangoni pa kaburi"

Bila shaka makaburi yale ya wakati wa Yesu ni tofauti na haya tuyaonayo hapa kwetu Afrika, hata kama tumeiga utamaduni  wa maziko na makaburi kwa mfumo wa Kikristo toka kwa wale waliotuletea Injili na kuanza Kanisa hapa Afrika Mashariki.

Wakati ule wa Yesu kaburi ilikuwa kama pango ambapo mlangoni lilifunikwa na jiwe kubwa kama la kusagia nafaka  ( kwa wale ambao bado wanaendelea na mfumo huo wa maisha). Mara nyingi jiwe la kinu cha kusagishia cha wenyeji ni kubwa sana. Tulikuwa nayo huku Moshi, Tanzania.

Katika safari ya kwenda kukamilisha maziko wanawake hao jasiri: Maria Magdalene, Maria wa Yokobo na Salome (kulingana na Injili ya Marko) waliona tatizo moja tu mbele yao,  ni jinsi ya kuliviringisha jiwe lililokuweko mlangoni mwa kaburi, nao waweze kuingia na  kumpaka Bwana wao mafuta, watoe heshima zao za  mwisho na kuhakikisha mwili  ( maiti yuko amehifadhiwa vizuri.).

Wanawake hao ni jasiri kwani hawaonyeshi kuogopa au kutishwa na maaskari waliokuwa wakilinda doria na hasa baada ya kuuwa Yesu na kuzikwa (Mt. 27: 60 - 61) Mt. 27:65 - 66), ulinzi mkali!

Walijua Yesu ni Bwana na mfalme. Alihitaji heshima hata kama wengine walimdharau na kumtesa Mariamu alikuwa na wosia wa Yesu ambao bado kuutekeleza ( "... Mwache aiweke kwa siku ya maziko yangu") (Yn. 12:3 - 8)

Ajabu, Habari njema zinawajia bila wamama wale kutazamia.  Kwa mshangao wanakuta jiwe lile kubwa limeondolewa tayari. Ehu! Hii ni ishara njema ya matumaini, kikwazo kikuu kimeondolewa.  Lakini wanapochungulia ndani ya kaburi sasa hawaoni mwili wa marehemu.  Hili ni tatizo baada ya matumaini ya kuvuka kizuizi/kikwazo cha kwanza cha jiwe kubwa.  Hata hivyo, Habari Njema tena wanapoipata baada ya muda mfupi tu.  Malaika wa Mungu (sura kama kijana) anawapa matumaini mengine makubwa zaidi.: Mnamtafuta Yesu... amefufuka hayupo hapa, patazameni walipomweka.  Lakini enendeni zenu, mkawaambie wanafunzi... awatangulia kwenda Galilaya, huko mtamwona kama alivyowaambia (Mk. 16:7).  Hizi ndizo habari za uhakika kwamba Yesu amefufuka kweli kweli.  Tena ni Habari Njema kwamba Yesu ameshinda kifo, kaburi na nguvu za shetani.  Yeye ni hai na yu hai akiwa limbuko letu Wakristo pamoja nao waliokufa katika imani.


III. Mambo ya Kutafakari Sisi Wakristo wa Leo Katika Kuadhimisha Pasaka:   Ufufuo wa Yesu

Kuna jiwe gani linalokutisha, linakuwia kikwazo cha kuendelea kukua na kufurahia uzima unaopata kwa Wokovu wa Kristo? Kuna jiwe gani linalokuzuia katika utendaji wako wa kazi, masomo na maisha?

Yako mawe makubwa na madogo ambayo yaweza kuwa kikwazo cha kutimiza Ibada na ufuasi wetu na kutuzuia kuonyesha upendo labda majeraha au makwazo ya viongozi, au makwazo katika familia na ndoa zetu? Labda makwazo toka walimu au wenzi na ndugu zetu?

Labda tabia zetu wenyewe zilizoacha maadili tunayofundishwa toka neno la Mungu kupitia neno lake, ambalo lina pande mbili Sheria na Injili.  Twahitaji kumulikwa na sheria na amri za Mungu mfano: Ulevi, uzinzi, wizi, choyo, ulafi, kiburi, dharau nk.

Twahitaji kujutia makosa/dhambi zetu.  Lakini kwa kuwa sheria haziokoi bali kutuhukumu basi tukimbilie kwa Yesu.  Na tusikie jinsi anavyoita na kutualika sisi akisema, Njooni kwangu ninyi nyote msumbukao na kulemewa na mizigo nami nitawapumzisha (Mt. 21:25ff).  Tena Yesu anatuhakikishia leo akisema, mimi nimekuja ili wawe nao uzima tele Yn. 10:30 kila ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe.

 

IV. Mwisho

Leo ni Pasaka I, Habari Njema kwetu ni za Ufufuo Yesu Kristo Amefufuka kweli Haleluya.  Yeye ni limbuko lao waliolala/waliokufa kimwili wakiwa katika imani (Yn. 12:26), maana nao watafufuliwa ili kumlaki Yesu Kristo atakapokuja kulichukua Kanisa mbinguni. Wanawake jasiri watatu, wamekuwa ndio shuhuda wa kwanza kutuletea habari Njema za Ufufuo. Hao wanaitangaza Injili pamoja nasi sote bila ubaguzi.  Malaika akawaambia, mnamtafuta Yesu Mnazareti aliyesulubiwa, amefufuka hayupo hapa kaburini tena.  Sasa Yesu yuko mbinguni ndio Galilaya ya mwisho ambako sote tuliompokea na kumwamini, tutakutana naye pamoja na Petro. (Yn. 1:12f), baada ya maisha haya.  Turudi nyumbani, mahala pa kazi shuleni, na katika jamii tukamtumikie kwa furaha na shukrani ya Ufufuo limbuko letu ( Zab. 100).  Ameni!

 



Dawson E. Chao
Chuo cha Theologia na Biblia Mwika,
S.L.P. 3050,
MOSHI - TANZANIA.
E-Mail: dawsonchao@yahoo.com

(zurück zum Seitenanfang)