Göttinger Predigten im Internet
ed. by U. Nembach, J. Neukirch, C. Dinkel, I. Karle

Siku ya Watakatifu 05 Nov. 2006
NENO KUU - UENYEJI WA MBINGUNI
Israel Y. Natse
(->current sermons )


Neno la Mahubiri ni kutoka I Thes. 4:13-18
Na Mch. Israel Y. Natse

“Lakini, ndugu hatutaki msijue habari zao waliolala mauti, msije mkahuzunika kama na wengine wasio na matumaini. Maana, ikiwa twaamini ya kwamba Yesu alikufa akafufuka, vivyo hivyo na hao waliolala katika Yesu, Mungu atawaleta pamoja naye. Kwa kuwa twawaambieni haya kwa neno la Bwana, hakika hatutawatangulia wao waliokwisha kulala mauti. Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa na Bwana milele. Basi, farijianeni kwa maneno hayo. (SW UV).

Wapendwa wasomaji wangu, leo ni siku ya Watakatifu kulingana na kalenda yetu ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na matafakuri kwa juma zima linaloanza leo ni juu ya UENYEJI WA MBINGUNI, maana yake maisha baada ya maisha ya hapa duniani.

Katika habari hii, Mtume Paulo anatuangaliza katika mambo yafuatayo:-

I. TUSIWE KAMA WATU WASIO NA MATUMAINI

Mpendwa unayesoma habari hii, Mtume Paulo anawafariji Wathesalonike wanaohuzunika kwa sababu ya vifo vya marafiki zao wale waliokufa katika Kristo. Mtume Paulo anawakumbusha habari ya maisha baada ya maisha haya,. Paulo anawaambia kwamba, ikiwa twaamini ya kwamba Yesu alikufa akafufuka, vivyo hivyo na hao waliolala katika Yesu, Mungu atawaleta pamoja naye. Hii inatuonesha wazi kwamba sisi tulio wafuasi wake -- Wakristo hatuna sababu ya kuhuzunika wala kuogopa kifo, maana Yesu ameshinda kifo – Yu hai – Nasi ni Hai katika yeye.. Bwana Yesu asifiwe.

Mtume Paulo anatutia moyo kwamba hatuna sababu ya kuhuzunika kama wengine wasio na matumaini. Yesu ni tumaini letu. Mpendwa msomaji wangu Paulo anakaza juu ya maisha mazuri ya baada ya kufa – kufa katika Yesu Kristo. Na Yesu mshindi wa mauti anasema: Amin, amin, nawaambia, yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyempeleka yuna uzima wa milele, wala haiingii hukumuni bali amepita kutoka mautini, kuingia uzimani (angalia liturgia yetu ya mazishi). Kwa hiyo kifo/mauti kwa mkristo ni njia/daraja la kutuvusha kwenda uzimani – hatuhitaji kuhuzunika mara wapendwa wetu wanapoitwa. Ila kifo kitukumbushe kujiandaa kwamba hapa duniani sisi tu wasafiri na wapitaji – hatuna makao ya kudumu. Kesha kwa kuwa hujui saa na wakati atakapokuja mwana wa Adamu.

II. WOTE WALIOKUFA WATAFUFULIWA KWANZA

Kuna usemi wa kiingereza usemao, “First in first out”

Mpendwa msomaji wangu, Mtume Paulo anakaza juu ya ujio wa pili wa Bwana wetu Yesu Kristo. Anatuhakikishia kwamba wafu watafufuliwa kwanza, tena anasema, hakika hatutawangulia wao waliokwisha kulala mauti – maana yake hao wataamshwa kwanza ndipo tukamlaki Bwana hewani. Huu ndio ukweli wenyewe hatuna sababu ya kuwa na mashaka. Bwana wetu Yesu Kristo anasema, Amin, amin, nawaambia, saa inakuja na sasa ipo, wafu watakapoisikia sauti ya Mwana wa Mungu, na wale waisikiao watakuwa hai. Hii ina maana wote watafufuliwa, nao watatoka, wale waliofanya mema kwa ufufuo wa uzima na wale waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu. Hivi ndivyo tunavyoamini na ndivyo ilivyo katika liturgia yetu.

Mpendwa msomaji wangu neno kuu la juma hili ni Uenyeji wa mbinguni. Mtume Paulo anatueleza uzuri wa maisha baada ya maisha haya. Tena anatueleza kwamba uzuri huo uko katika Yesu Kristo. Hivyo mpendwa unayesoma habari hii ninapenda kukumbusha kuwa maisha ya sasa ni maandilizi ya maisha ya baadaye, uzuri na furaha ya maisha ya baadaye – mbinguni ni kuwa na Bwana (Yesu). Umwone Yesu katika maisha yako. Uishi naye na kumfurahia kwa maisha yako yote. Kwa kifupi umpe Yesu maisha yako ayatawale. Bwana akujalie kuona hivyo. AMEN.

Rev. Israel Y. Natse,
Principal
Mwika Lutheran Bible College ,
Moshi – Tanzania
isnatse@hotmail.com
isnatse@elct.org

 

 

 

 


(top)