Göttinger Predigten im Internet
ed. by U. Nembach, J. Neukirch, C. Dinkel, I. Karle

3 rd Last Sunday 12 th Nov. 2006
A Sermon by Grayson Z. Mtango based on Mark 13:32-37
(->current sermons )



Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba na ushirika wa Roho Mtakatifu ukae nanyi nyote. Amen.

Sala: Bwana Yesu Neno lako ndio kweli tutakase na kweli yako. Amen

Kichwa: MWENYE KUVUMILIA HATA MWISHO NDIYE ATAKAYEOKOKA

Shabaha : Wasikilizaji wasaidiwe kuishi maisha ya uvumilivu na kuwa tayari kumpokea Mfalme, Mwokozi wetu atakapokuja kulichukua Kanisa lake.

Utangulizi:
Wapendwa, Biblia inasema wazi chochote atakachopanda mtu ndicho atakachovuna. Je unajitayarishaje kumpokea Yesu Kristo atakapokuja kuwachukua wateule wake watakatifu?

Yesu Kristo Atarudi Tena:
Neno tulilosoma linatupa ukweli kuwa Bwana wetu Yesu Kristo atarudi tena katika maisha haya.

Siku ya kuja kwake haijulikani kwa mtu awaye yote, wala malaika isipokuwa Mungu Baba peke yake.

Kutokana na ushuhuda huu, hakuna sababu ya kukaa na kutafuta au kuangalia ratiba kuwa Bwana Yesu atakuja lini! Muhimu ni kuishi maisha kama yale ya watumwa wanaomngojea Bwana wao bila ya kujua ni muda gani atarudi.

Yatupasa Kumngoja Kristo:
Tumekwisha jifunza kuwa Bwana Yesu atarudi katika siku inayojulikana kuwa ndiyo ya mwisho. Siku hiyo itakuwa ya vitisho na mahangaiko mengi. Wale ambao hawakujiweka tayari na wasio na imani thabiti watayumbishwa na wala hawatajua la kufanya. Watabaki wakishangaa, kulia, kuhangaika, kushikwa na hofu nyingi isiyowasaidia kamwe. Ni muhimu kujua kuwa maisha yako unayoishi sasa ndio matayarisho ya kuingojea hiyo siku ya Kristo, siku ya furaha na kilio. (Ling: Mt. 7:21-23).

Kile mtu anachopanda ndicho atakachovuna. Wale wote wanaopenda dunia na tamaa zake, au kuzifuata tamaa za miili yao, ni wazi kuwa siku hiyo ya Bwana watavuna uharibifu (soma Galatia 6:6-8, Ling. I Yohana 2:15-17). Matendo ya mwili ni dhahiri ndio haya: Uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi na mambo yanayofanana na hayo (Galatia 5:19-21).

Mtu anayeyatenda hayo ni wazi kuwa anachofanya ni kupanda uharibifu na siku ile Bwana atakapokuja kuwachukua wateule, hatapata nafasi ya kumfurahia katika utukufu wake.

Nafasi ya Kujitayarisha kwa Upya :
Maisha yetu yote ni matayarisho ya kukutana na Mfalme. Je wewe ndugu na dada unayeusikia ujumbe wa Neno hili la Mungu unajitayarishaje kumpokea Kristo atakapokuja kulinyakua Kanisa lake.

Hakuna nafasi ya kuhofu, yachunguze maisha yako kwa msaada wa Roho Mtakatifu. Ikiwa kuna mahali ambapo maisha yako hayana ushuhuda wa wewe kuitwa Bibi Arusi aliye tayari kumngojea Bwana wake ajapo, basi chukua hatua ya imani. ya kutubu, kumwamini na kumrudia Yesu kwa upya.

Furaha tuliyonayo ni hii, Bwana Yesu hataki hata mmoja wetu apotee, bali wote tufikie mwisho ule mzuri wa kuishi naye milele (I Tim. 2:3-4).

Hitimisho:
Ninapofikia mwisho wa mahubiri haya niseme tena maneno haya “Chochote mtu atakachopanda ndicho atakachovuna”. Je maisha yako yanatawaliwa na kitu gani? Tukumbuke kuwa mwenye kuvumilia mpaka mwisho, ndiye atakayeokoka. Unatazamia kuvuna nini katika siku ile ya Kristo Yesu?

Niwakumbushe tena kuwa, vile mtu anavyoishi sasa, ndivyo atakavyoweza kufurahia au kuikosa furaha ya uzima wa milele. Basi ni nafasi nzuri kwa kila mmoja wetu aliyeusikia ujumbe huu wa Neno la Mungu kumwomba Mungu amsaidie kusimama imara na kuvipiga vile vita vizuri vya imani, ili siku ile Bwana wetu Yesu atakapokuja kulinyakua kanisa amkute akiwa tayari kumpokea kwa furaha na shangwe kuu.

Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu. (Filipi 4:7)

Sala:
Bwana Yesu tunakushukuru kwa Neno lako tulilolisikia. Tusaidie ili lituumbie imani thabiti ya kumtumaini na kumtegemea Kristo. Na atakapokuja, atuchukue, tukaishi naye katika raha ya milele. Amen.


Rev. Grayson Z. Mtango,
Mwika Bible College,
P.O. Box 3050,
Moshi

E-mail: mwika@elct.org


(top)