Göttinger Predigten im Internet
ed. by U. Nembach, J. Neukirch, C. Dinkel, I. Karle

JUMAPILI TAREHE 10 DESEMBA, 2006 SIKU YA BWANA YA PILI
KATIKA MAJILIO
MAHUBIRI KUTOKA INJILI YA MARKO 13:24-27
“BWANA ANAKUJA KATIKA UFALME WAKE”
(->current sermons )


Mara nyingi watu wa Mungu hasa sisi Wakristo tumepata kuhubiriwa na hata kujisomea wenyewe katika maandiko ya Biblia kuhusu matukio ya siku za mwisho. Mwanzoni mwa sura hii ya Injili ya Marko (13:1-4) Yesu anawadhihirishia wanafunzi wake ya kwamba fahari kubwa ya lile Hekalu la Yerusalemu itatoweka kwa kuwa litabomolewa. Wanafunzi wanamwomba awaaambie ishara zitakazotangulia tukio hilo. Yesu anawaambia kwamba patainuka manabii wa uongo, vita, matetemeko ya ardhi na njaa, lakini anawatahadharisha ya kuwa hayo yote hayana budi kutokea bali ule mwisho bado. Anafananisha matukio hayo kama dalili za maumvu ya kwanza tu kwa mama anayetarajia kujifungua mtoto

Dalili za kutisha na za ajabu zitaonekana wakati wa kuja kwake Yesu Kristo. Tunapotazama jua, mwezi na nyota mbinguni, kwa mtazamo wa kibinadamu tunafikiri kwamba zitaendelea kudumu milele. Tulianza kuziona tokea tuzaliwe na hata sasa zipo na bado tunaendelea kuziona. Yesu Kristo anatuonya yeye mwenyewe ya kuwa itakuja siku ambayo alimwengu huu utakwisha. Somo hili la leo linatuonyesha jinsi ambavyo jua litatiwa giza, mwezi hautatoa mwanga tena, nyota zote zitaanguka na nguvu za kimbingu zitatikisika.

Neno linatuambia ya kuwa dalili hizo za kutisha za siku ya kurudi kwake Bwana Yesu zitaambatana na dhiki kuu. Neno ‘ole’ linatumika (13:17) likiwa na maana ya kuwa patakuwepo na shida kubwa au mateso makali, ambayo hayajapata kutokea tena tangu kuumbwa kwa ulimwengu mpaka leo hii na kwamba hayatatokea tena kamwe. Bwana wetu Yesu Kristo anabainisha ya kuwa mateso na shida hizo ni kwa wale ambao watakuwa hawajampokea yeye kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yao.

Baada ya dhiki kuu, Neno hili linatuambia kwamba Mwana wa Adamu atakuja kutoka mawinguni kwa nguvu nyingi na utukufu (13:25,27) na ndipo atakapowatuma malaika kuwakusanya wateule wake toka pande zote za dunia. Wateule wa Mungu hawatakuwa watu wa taifa moja tu bali ni watu wa mataifa ya ulimwengu wote, ni wale wote waliomkubali Yesu Kristo, wakamwamini, wakamtumikia na kumtegemea yeye peke yake. Siku hii itakuwa ni siku ya utimilifu wa haki na upendo wa Mungu kwa watu wake. Ni dhahiri kwamba katika maisha yetu leo hapa ulimwenguni wapo watu wakubwa na wadogo, tajiri na maskini, wanyonyaji na wenye kunyonywa, wanaoonea na wanaoonewa, lakini tunaambiwa kwamba hali hizo zote zitakoma siku hiyo. Waovu wote watapata adhabu yao na wafuasi waaminifu wa Yesu watapata tuzo yao; kwa maana kukubaliwa na kukataliwa kwake Yesu Kristo ndiyo ilikuwa dhamira kuu ya Injili, hivyo mateso na utukufu ni dhamira ile ile kwa maneno mengine.

Neno la Mungu linatuonya sisi Wakristo tusijisumbue kujua ni lini dunia itaangamia. Jambo muhimu na la msingi ni kuamini na kutambua kwamba mateso na dhiki ya ulimwengu huu yatakuwa na kikomo chake. Yesu Kristo kwa kinywa chake mwenyewe anakiri akisema, “Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe. Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba”. (13:31,32). Wakristo tujue kwamba Yesu atawajia wale watakaoweza kuvumilia hata mwisho kwa kuwa ndio watakaookoka. Tunahitaji uvumilivu mkubwa pamoja na maombi na sala katika kipindi hiki kigumu cha kusubiri msaada wa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo.

Yesu Kristo anawaasa wanafunzi wake wawe macho na wakeshe ili atakapokuja ghafla asije akawakuta wamelala (13:36). Vivyo hivyo na sisi sote inatupasa kukesha tukidumu katika maombi na toba ya kweli itakayotupatia wokovu. Tutambue kwamba mafundisho yote ya Yesu yalikuwa ya kweli na makamilifu. Yesu hakutoa kamwe mafundisho yenye makosa kuhusu ujio wake wala kuhusu neno lolote. Alitamka bayana ya kuwa alijinyima utukufu wake wa Kimungu kwa muda hata akafanyika mwili. Hivyo yote aliyofundisha aliyafundisha kwa mamlaka ya Kinungu na bila makosa yoyote.

Wajibu tuliopewa na Yesu sisi Wakristo ni kuwafundisha wale wengine wote wasiomjua Yesu waweze kumjua na kumwamini na kumfuata. Tunaitwa kuifanya kazi hiyo kwa uaminifu. Tatizo kubwa tulilonalo sisi wanadamu ni kwamba tunayo mioyo migumu mno kukiri na kuamini katika baadhi ya mambo hasa hili la nyakati za mwisho. Inatupasa tujiweke tayari sisi wenyewe kwanza kabla hatujajaribu kuwasaidia wengine kuwa tayari. Huo ndio wajibu wa kila mtumishi na kila Mkristo mwaminifu. Tujiweke tayari kwa kumrudia Bwana na kuungana naye ili atakapokuja tumjue yeye naye atujue sisi.

Kwa kuwa Mungu ndiye Mtawala wa mambo yote, saa ya kuja kwa Mwanae imo mikonini mwake mwenyewe. Sisi wanadamu hatuwezi kuiharakisha wala kuiahirisha. Wale waliojaribu kuiharakisha hakika waliangamia vibaya. Baadhi yetu tunakumbuka vema habari za mtu mmoja aliyeitwa Kibwetere na wafuasi wake wa nchini Uganda walivyojiangamiza wenyewe walipokidhania kwamba tarehe 31 Desemba, 1999 ingelikuwa siku ya mwisho wa dunia na haikutimia hivyo. Mamia ya watu waliteketezwa kwa moto katika hakalu lao na wengine kuuawa kikatili sana na kuzikwa katika makaburi ya pamoja. Bila shaka wengi wao hawakuwa tayari kwa ajili ya siku hiyo ya Bwana waliojipangia wao wenyewe.

Tuifanye kazi ya Bwana kwa imani bila hofu au masiwasi tukitambua kwamba tunaye Roho Mtakatifu wakati wote anayetufundisha na kutukumbusha yote tunayoopaswa kutenda kwa ajili ya utukufu wa Jina lake Bwana.

.Bwana atusaidie sisi sote ili tuweze kumpokea na kumshangilia katika mioyo yetu na katika maisha yetu yote ya ufuasi. Neno lake Bwana na libarikiwe. Amen.

Mchungaji Johann W. Kaale,
Ckhuo cha Biblia na Theologia Mwika,
S.L.P. 3050, MOSHI, TANZANIA
E-mail: Rev.kaalejohann@yahoo.com

 


(top)