Göttinger Predigten im Internet
ed. by U. Nembach, J. Neukirch, C. Dinkel, I. Karle

NEW YEAR’S EVE, January 1, 2007
A SERMON BY REV. DAWSON E. CHAO BASED ON JOB. 8: 8 – 22
(->current sermons )


Somo: Ayubu 8: 8 – 22
Neno Kuu: MUNGU HAMTUPI MTU WAKE
Kusudi: Wote wamtegemee Mungu pasipo shaka wakijua kwamba Mungu ni mwaminifu hatamtupa mtu wake nje, wachamungu na wote wanaomtegemea Yesu Kristo, atawabariki kwa wingi.

I. Utangulizi

Jea Ayubu ni nani?
Ni mtu mmoja mchamungu mtu mwenye sifa (mkamilifu), tena mtumishi tajiri mwenye ustawi mzuri (Ayub. 1 1 – 5). Kitu cha ajabu ni kuwa Mungu alimruhusu shetani amjaribu kwa mapigo na mateso mbalimbali ili apate kuona (shetani) kama ataendelea kumchamungu, kumtii Mungu na kumtegemea kuliko vitu vyote. (11:8 – 12). Ndipo tunaona wanamjia Ayubu, marafiki zake, Elifasi mtemani, Bildadi Mshuhi, Sofari mwamathi na baadae Elihu kumpa ushauri tofauti tofauti katika hali yake hiyo ngumu. Kama ilivyo kawaida ya watu katika hali kama hii ya mateso ambapo muathirika anahitaji faraja lakini, wengine wa marafiki wanmtonesha na kukatisha tamaa badal ya kumpa faraja katika hubiri hili tutajikita zaidi (mistari, 20 – 22). Hapa ni mwendelezo wa mahojiano kati ya Ayubu na rafiki zake kuhusu matatizo na majaribu yaliyompata. Ayubu wa leo anaweza kuwa ni wewe/mimi au mtu mwingine.

II. Mateso ni Sehemu ya Maisha Yetu

Hapa tunamwana Bildadi akihojiana na Ayubu juu ya adha inayompata ya majaribu. Kwake Bildadi anamkatisha tamaa Ayubu, kwani anadai kuwa:

(a) Mateso anayopata Ayubu mengi sana pamoja na familia yake. Hoja ya Bildadi kwa Ayubu ndio hii “ Ikiwa Mungi ni wa haki, naye anahukumu kwa haki bila shaka Ayubu anapokea haki yake ambayo ni adhabu anayostahili (ms 3 – 6)

(b) Kwa maneno mengine ni kwamba kama Ayubu angekuwa mtu mchamungu mwenye matendo mema yasingelimpata yaliomtokea katika familiayake. Kwa sababu Mungu huwabariki wenye haki lakini wasio haki huingia hukumuni na kuadhibia kwa maovu yao.

(c) Badala ya kumpatia faraja Ayubu basi Bildadi anamuongezea mzigo wa moyoni, uzito wa mawazo unamlemea.

(d) Fikra za namna ya akina Bildadi ni potofu na uzushi, kinyume na mafundisho sahihi ya imani ya Kikristo. Usahihi ni kwamba, mateso ni sehemu ya kawida ya maisha ya muamini Mkristo. Yako katika mpango mpana wa Mungu wenye kutimiza makusudio mema ya Mungu baadae.

(e) Tunaposoma Agano la Kale, watu mbalimbali walionja mateso ikiwa ni pamoja na manabii waliotenda na kutangaza mapenzi ya Mungu mbele za watu, mfano Yeremia 15 :10f, Hosea, Amosi, Elia nk. Hali kadhalika tunaposoma Agano Jipya tunaona jinsi Yesu na baadae mitume wake walivyopata mateso katika kushuhudia imani yao, tena katika utekelezaji wajibu zao. Biblia yatufundisha kuwa mfuasi wa kweli ni yule aliye tayari kukubali na kubeba msalaba (mateso) akimfuata Yesu Kristo (Mt. 16: 24 – 25). Mtume Paulo naye akionyesha faida ya mateso ya Kristo ambaye ndiye kielelezo chetu na tumaini letu asema, “ kwa sababu neno la msalaba kwao wanoptea ni upuuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa nai nguvu ya Mungu” (1 Kor. 1:18)

Yesu Kristo aliteseka bila yeye kuwa na dhambi au waa lolote , lakini aliingia mateso, majaribu na dhiki akawa mtiii hadi mauti ya msalaba (Fil. 2: 5ff). Na Mungu akamuadhimisha akampa Yesu jina lililo kuu kupita yote. Sisi wakristo hatuna budi kuepuka watu wenye mawazo na mafundisho potofu wakidanganya kwamba, kila ugonjwa au ulemavu watokana na dhambi, ama toka kwetu au wazazi wetu. Pengine watu wengine watatujaribu kwa kuorodhesha mafanikio walio nayo leo na kuwadharau maskini wanyonge kama ni ya halali, lakini wasikumbuke kwamba leo na kesho ni tofauti. Wako watu wanaojivunia mafanikio ya usitawi wa maish na uchumi na kuambatanisha na wokovu wao. Ati usitawi wao ndio kigezo cha kuthibitishia ulimwengu wokovu wao. Ni kweli yawezekana mambo mengine kama umaskini tukawa tumechangia kwa kutotimiza wajibu wetu. Lakini si mara zote Mateso ni sehemu ya maisha yetu. (Filp. 1: 29 – 30)

III Mungu Hatamtupa Mtu Wake Nje Kamwe

Katika mwendelezo wa mahojiano kati ya Ayubu na waliomtembelea ili kumpa ushauri, tunasoma pia habari za Eliabu, ambaye amempatia maneno ya faraja zaidi Ayubu kinyume na Bildadi katika mistari ya 20f. Neno la Mungu latufundisha ya kuwa Mungu hatamtupa mtu mkamilifu, na wala hatamtupa mtu wake nje, ndio maana Yesu akasema, kila ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe (Yon. 6:37). Naye nabii Yeremia anashuhudia hivi kwa Yer. 3:31ff, katika Biblia twasoma mwaliko wake Mungu kwetu akituambia, “njooni tusemezane, dhambi zenu zijapokua nyekundu zitakuwa nyeupe kama theluji…” (Isa. 1:18). Je, itakuaje Mungu amtupe mtu wake kama Ayubu mtu mkamilifu mbele yake? (ayub.1:1). Lakini pia Bwana hatawathibitisha waovu kuwa hawana hatia, la! Yeye Bwana anawaalika waje wote kwa Toba, waungame dhambi watu wote wakimwendea kwa imani namatumaini kwani hatamtupa yeyote nje kamwe. Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, msaada utakaonekana tele wakati wa mateso (Zab. 46:1 – 3). Ayubu alimwamini Mungu, alijua penye kimbilio lake ni kwa Mungu tu na siyo pengine. Ilibidi Ayubu kuteseka, kustahimili majaribu yote yaliyompata kusudi ajithibitishe kwa Bwana. Waswahili husema”Baada ya dhiki ni faraja”. Tunapoendelea kusoma habari za Ayubu hadi mwishoe utaona jinsi Mungu alivyomrudishia ustawi wake, baraka tele kwa watoto na mali, maradufu. (42: 7 – 17) baada ya kustahimili mateso.

IV. Habari Hizi za Ayubu Zatufundisha Nini?

(a) Mateso yake ni fundisho kwake yeye mwenyewe na kwetu pia, ya kwamba hakuna mtu awezaye kusimama na nguvu zake peke yake mbele za Mungu. Sisi sote tunamhitaji Mungu atuwezeshe na atupe nguvu ya kustahimili (Isa. 40:28 – 31)

(b) Tunapofika mwisho wa siku twamaliza mwaka wa 2006, pengine tuliishiwa nguvu njiani na kukata tamaa? Pengine tulipoteza njia/dira ya imani na kuanza kutangatanga? Lakini safari yetu bado ndefu tunapenda kwenda mbinguni. Turudi nyuma tuangalie ni wapi tumeanguka ili tukatubu, naye Bwana atatusamehe na kutupatia mwangaza na nguvu mpya ya kuendelea mbele. (Uf. 3:2 – 3).

V Tukate Shauri Kumtumikia Bwana

Hapa kabla ya kuanza tena siku mpya na mwaka mpya kesho 2007 na tukate shauri tena kama Yoshua. Tuwaalike wenzetu na wengine wote. “Chagueni hivi leo mtakayemtumikia pindi tukivuka mwaka huu na kuingia mwaka mpya (Yos. 24: 14 – 15). Yeye Yoshua mwenyewe akaweka msimamo wake bayana akasema tazama, mimi na nyumba yangu tutamtumikia Bwana, wala siyo miungu mingine (kumbuka amri ya kwanza). Iko hatari kumwacha Bwana ni maangamizi (Yos.24:20).

Mwisho

Ayubu alimcha Mungu, akamtii hata wakati wa majaribu na mapigo ya shetani, hatimaye alishinda na kurudishiwa mara dufu baraka tele. Kielelezo kikubwa zaidi kwetu ni Yesu Kristo mwenyewe. Yeye asiyekuwa na dhambi alifanywa kupokea hatia ya dhambi akahukumiwa kifo na kutii hukumu hiyo ka ajili yetu. “ Sasa basi, hakuna hukumu ya kifo juu yao walio ndani ya Kristo Yesu … (Mdo. 8:1ff) Hizo ni habari njema kwetu sote tunaopenda kumtii Bwana. Tuepuke wanaopotosha na kukatisha tamaa bali tumtazame Yesu tu mwenye kuanzisha naye ataikamilisha imani yetu. Amen!

Rev. Dawson E. Chao,
Mwika Theological College,
P.O. Box 3050,
MOSHI – TANZANIA.
E-mail: mwika@elct.org
Dawsonchao@yahoo.com

 

 

 


(top)