Göttinger Predigten

deutsch English español
português dansk Schweiz

Startseite

Aktuelle Predigten

Archiv

Besondere Gelegenheiten

Suche

Links

Gästebuch

Konzeption

Unsere Autoren weltweit

Kontakt
ISSN 2195-3171

Göttinger Predigten im Internet hg. von U. Nembach

Third Sunday of Easter, 22.04.2007

Predigt zu Ezekiel 34:10-19, verfasst von Peter Msengi

Mimi ndimi Mchungaji mwema, Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo.

Utangulizi

Miongoni mwa watu wa Yuda waliopelekwa kifungoni Babeli mwaka wa 597 BC alikuwa kuhani kijana wa umri wa miaka 25 tu, wakati wa Ezekiel nchi ya Palestina ilikumbwa na mabadiliko makubwa ya kisiasa, kidini na kiuchumi pia, kwa sababu  Dola ya Babeli ilitumika na kuangamiza Yerusalemu na kuwachukua mateka Waisrael ambao ndilo Taifa la Mungu.  Ezekiel alifikiri maisha ya utumwa yangekuwa mafupi na hivyo angerudi Yerusalemu na kutumika kama nabii huko.  Lakini baada ya miaka mitano hivi Mungu alimjulisha kuwa asingerudi Yerusalemu, hivyo angepaswa kufanya  unabii kwa Wayahudi walioko Babeli. (Ezek. 1: 1- 3) 2:3,5,7) 3:4).  Mahubiri yake ya Unabiii yalidumu kwa miaka  22 ( Ezek. 25:17).

Kazi za Nabiii Ezekiel - Babeli

Ezekieli alipoanza kazi ya kutoa unabii alilaumu maisha ya dhambi yaliyofanywa na watu wa Mungu (Israel) kule Yerusalemu, pia aliwatangazia ukombozi kwa mji wao Yerusalemu.  Ezekiel aliweka wazi kuwa wao wamechukuliwa utumwani (mateka) hiyo ni hukumu ya haki kwao iliyofanywa na Mungu.  Lakini wasikilizaji wa mahubiri/unabii wake walikataa kumkubali wakidai kuwa Yerusalemu kutokombolewa mapema labda kizazi kijacho (Eze. 12: 27 - 28).

Hata hivyo Ezekieli alitiwa moyo aendelee kuwaandaa Waisraeli kiroho kwa ajili ya wakati mpya ambao Mungu aliwaahidi kwani imani yake na tumaini lake lilikuwa kwa Mungu ya kwamba Mungu atawasamehe dhambi na kuwapa nafsi tena ya kumrudia yeye Mungu wa kweli na kumtumikia kwa moyo wa upendo.

Kulingana na hali ya mateso yaliyosababishwa na viongozi wabaya wa wakati wa  nyuma Taifa lilijenga matumaini ya kwamba Mungu atawapa serikali bora kwa wakati wa baadaye. (Ezek. 34: 1 - 31).

Kutokana na matumaini hayo ndipo Ezekiel anajenga mahubiri yake kwa taifa la Israel lililoko ugenini akiwaambia kuwa, Bwana Mungu amesema yeye ni juu ya wachungaji maana yake ndiye mkuu wa watawala wote.  Hivyo watawala/ viongozi watadaiwa  wale watu (kondoo) mikononi mwao.  Mungu anasema atawaondoa madarakani ( kuwaachisha kazi ya kulisha kondoo).  Hivyo hawataendelea kujinufaisha wenyewe kwa kuwatumia kondoo wa Bwana.  Bwana Mungu anasema atawaokoa kondoo katika vinywa vyao, ili wasiendelee kumalizwa.

Mungu aliye mchungaji mwema anasema atawatafuta kondoo zake ( watu wake, taifa lake) liliko ugenini na utawanyikoni.  Mungu anaahidi kuwatoa kati ya mataifa na kuwakusanya na kuwapeleka katika nchi yao wenyewe (nyumba au zizi).  Kazi ya Mungu aliye mchunga mwema ni kuwapatia malisho mema na kuwapa maji safi, kuwapa mahali pa kupumzika na kutulia katika nchi yao.  Kazi ni kuwatafuta waliopotea na kuwarudisa walikofukuzwa, kutoa huduma kwa wagonjwa na walioumia (kukata tamaa, kuvunjika moyo) bali nitatoa hukumu kwa wasio haki.  Ezekiel anauliza Je Mungu kuwahudumia ninyi ni neno dogo?  Wale kondoo na mbuzi dume walionona wamefanya kiburi na jeuri kula na kutumia maji kisha kuyavuruga ili wale wanyonge wakose malisho mema na maji safi.

Ujumbe wa Kanisa la Leo

Ukisoma Yeremeia 23: 13 - 15 Mungu anasema ameona viongozi wabovu huko Samaria wanaotabiri kuhusu Baali badala ya Yahweh Miungu badala ya Mungu.  Hii ndiyo hali iliyopo leo Kanisani na hata viongozi wa nchi pia.  Manabii wa Yerusalemu wamefanya chukizo sana kwa sababu wamefanya zinaa, wamesema uongo, wamewapendelea watenda maovu watu wasio haki na hata watu wameshindwa kumrudia Mungu na kuacha uovu wao.  Hali hii imelikumba Kanisa, viongozi wa Kanisa wametumbukia katika uzinzi, wizi, uongo na mambo yasiyo ya haki na kupendelea watu.  Nguvu yao ni rushwa ambayo imewapotosha kutenda haki na kweli.

Viongozi Kutowajibika Katika Uongozi Wao

Marko 11 - 16 Mungu amechoshwa na hali hiyo mbaya hivyo anachukua wajibu yeye mwenyewe wa kutunza na kuhudumia kundi lake. Isa. 40:11 yeye ajuae kuwainua wanyonge na kuwatia moyo na kuwaganga wale waliovunjika. Yer. 31:10.

Mpendwa kiongozi wa Kanisa la Mungu Mchungaji, Askofu, Mwinjilisti, Mzee wa Kanisa na wengine wote mlio na wajibu Kanisani na hata serikalini hebu angalieni Je mnatenda haki na kama hutendi haki na kutimiza wajibu kama ikupasavyo Mungu amemuandaa yule mnyonge ili amkabidhi kazi hii ndivyo asemavyo

(2 Sam.12:1 - 15). Daudi alitubu dhambi yake kwa Bwana naye akatangaziwa msamaha. 

Ni imani  kuwa viongozi wa Kanisa wameshindwa kukumea na kutimiza haki za jamii aidha kwa kuhofia maisha yao na pengine wao wenyewe kuwa washiriki wa maovu hayo katika jamii mfano leo hii rushwa ni kikwazo kikubwa cha kutendeka haki kwa watu wanyonge pia, dhuluma, uonevu, wizi, biashara haramu kama za madawa ya kulevya yanafanywa na watu wenye uwezo kifedha na mamlaka.  Je Kanisa limewataja na kuwadhihirisha wazi ama viongozi wameogopa kupoteza nafasi zao. Je tume ya kuzuia rushwa na sheria za bunge zimefuatilia kikamilifu ili kuondoa mwanya wa rushwa katika utekelezaji wa haki katika jamii au yamefanywa mambo mazuri kwa maneno tu bali utekelezaji umeshindikana kwa kuhofia maisha.

Tukumbuke Yesu anaposema mimi ndimi Mchungaji mwema na mchungaji mwema hutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo wake.  Kiongozi wa kweli ni yule aliye tayari kupoteza maisha kwa ajili ya kundi lake.  Ni yule anayeshiriki maumivu na machungu ya wanyonge na siyo anayejitanguliza nafsi yake.  Viongozi hawa ni wachinjaji wa kondoo na wala si watunzaji.  Kiongozi ni mhudumu na siyo mhudumiwa, Je wewe uliye kiongozi unayo tabia gani katika wajibu uliopewa na Bwana kama Mchungaji na mlinzi wa haki na msimamzi wa huduma zote basi ukiwa huwezi achia nafasi ya uongozi ulio nayo kwa sababu Mungu amesema atawataka wote mikononi mwako.

Hebu angalia kundi ulilokabidhiwa umelikusanya au limetawanyika, Je unajifahamu kuwa wewe ndiyo chanzo cha hali yoyote inayokabili kundi ulitunzalo?  Nikutie moyo kuwa Mungu anaifahamu kazi yako ikiwa mbaya au nzuri naye atakuhukumu sawaswa na nitendayo.  Tubu ili ili Mungu akusamehe dhambi uliyo nayo na uombe Mungu akupe hekima ya Uongozi.

Tuombe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo tunahitaji huruma yako kwa udhaifu tulionao hasa viongozi wako uwape moyo wa kulichunga vema kundi lako. Amen!

 Rev. Peter Msengi

E-Mail: mwika@elct.org

(zurück zum Seitenanfang)