Göttinger Predigten

deutsch English español
português dansk Schweiz

Startseite

Aktuelle Predigten

Archiv

Besondere Gelegenheiten

Suche

Links

Gästebuch

Konzeption

Unsere Autoren weltweit

Kontakt
ISSN 2195-3171

Göttinger Predigten im Internet hg. von U. Nembach

2. Sonntag nach Trinitatis, 17.06.2007

Predigt zu Nehemia 2:17-18, verfasst von Mch Dawson E Chao

 

Neno Kuu: NA TUONDOKE TUKALIJENGE KANISA LA BWANA.

Kusudi: Waamini wote wawe na Umoja (Yn. 17:21), wote wapate mwamko mpya wa ari ya kwenda kumshuhudia Yesu Kristo mbele ya watu wote, na kulijenge Kanisa la Bwana, liwe chumvi na nuru ya ulimwengu wote, na kumtukuza Mungu. (Mt. 5: 13 - 16).

I. Utagulizi:

Leo ni sikukuu ya KKKT, yaani Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, ambalo limefikisha miaka 44 tangu lilipozaliwa mwezi June 1963.  Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania lenye waumini wapatao milioni 3.5, limezaliwa kwa kuunganisha yaliyokuwa makanisa saba (7) ya Kilutheri yaliyotokana na vyama vya Kimisioni toka Ulaya na Marekani, kabla ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Tanzania mwaka 19964.

Makanisa hayo yaliitika na kutii wito wa Yesu Kristo, ya kuwa wote wawe na Umoja (kama Yeye na Baba walivyo), ili nao ulimwengu upate kusadiki utume wao. (Yn. 17:2).  Tunamshukuru Mungu kwa kazi hii nzuri iliyofanywa na viongozi wa makanisa hayo kutafuta umoja wenye nguvu kwa ajili ya kazi ya Missioni, pamoja na vyama anzilishi vya makanisa hayo.  Waliona mbali kwa mwangaza wa Roho Mtakatifu, wakasahau na kushinda ubinafsi, wakatazama  manufaa ya kazi ya Bwana, ambayo kweli matunda yanaonekana katika nchi ya Tanzania hadi majirani, ambako moto wa Injili unaendelea kutapakaa ikitokea Tanzania, kwa msukumo wa wakristo walei ama waliotoka na kuhamia nchi jirani, au kwa njia ya majirani walioishi hapa kwetu, bila kusahau wakimbizi, ambao wanarejea na kuanzisha/kuendeleza Kanisa kule kwao.  Baadhi ya wakimbizi wamekuwa chombo muhimu kwa uenezi wa Injili ya Yesu Kristo hapa Afrika.  Mtume Paulo anasema, "Kila atakayeliitia jina la Bwana (Yesu) ataokoka... Bai imani chanzo chake ni kusikia, na kusikia huja kwa neno la Kristo'' (Rum. 10: 9, 13, 14 - 17).

Kanisa (KKKT) limeungana pia na Makanisa mengine na kuanzisha Jumuiya ya Kikristo Tanzania (JKT), yote haya ni kutimiza wito wa Yesu Kristo, wa Umoja ni Nguvu, na hii imetuwezesha kushuhudia pamoja mbele ya tawala za kidunia (jamii) na mbele yao mataifa, nao walio nje ya imani ya Kikristo, hata  wakiwa ni watu wa dini mbalimbali.  Utume wa Yesu Kristo ni kwa watu wote pasipo ubaguzi wa aina moja au nyingine.  Kila binadamu anayo haki ya kusikia Injili toka wajumbe/wafuasi na mamlaka yale yalioagizwa na Yesu Kristo (Mt. 28:19) kufikisha utume wa Injili ndio wajibu na msingi wa Kanisa lote, KKKT ikiwemo kama sehemu ya Kanisa Katholiko au la ulimwenguni pote na kwa wakati wote). Uamuzi wa kukata shauri na kumpokea Yesu Kristo   kama Bwana na Mwokozi, unabaki kwa yule aliyesikia Neno la Mungu, yaani mlengwa wa missioni. Kanisa linaanza mara baada watu kupokea ujumbe na kukata shauri  na kumkiri  Yesu Kristo.  Ndipo waliobatizwa huanza kulijenga Kanisa la Mungu lililoanzishwa ndani yao na Roho Mtakatifu.

Je, Kanisa ndio nini? Kwa muktadha huu, Kanisa ni kusanyiko  la watu walioitwa na Roho Mtakatifu, ambao ndani yao Neno la Mungu lahubiriwa kwa usahihi na sakramenti zinatolewa kulingana na  Injili yenyewe (Mdo. 2: 38, 41f; 2:46). Tena kanisa ni la Bwana, sisi ni washirika kwa neema tu.

 II.  TUKALIJENGE KANISA LABWANA

Katika somo la leo (Neh. 2:17 - 18) tunakutana na mfano kielelezi kwa watumishi wa Bwana huko Yerusalemu na Uyahudi kwa ujumla.  Watumishi hao ni Ezra na Nehemia.  Ingawa somo letu lahusu Nehemia zaidi, ni vizuri tukaona habari za watimishi hao na walivyohusiana ujenzi wa Hekalu, Yerusalemu na kuta zake, na taifa kwa jumla.  Tunaposema AK, katika Biblia twaona ya kuwa kitabu cha Ezra na kile cha Nehemia vinafuata na si tu kwa mpangilio, bali na mambo yaliyomo au yaliyotendeka.  Kiini cha vitabu hivi ni kujenga upya: Hekalu na mji wa Yerusalemu ambavyo ni kama moyo na mwili wa utaifa wa Uyahudi na Israeli kwa ujumla.  Taifa teule limekuwa na nafasi pekee katika mahusiano ya watu wa Mungu.  Mungu wa kweli, Yahweh (Bwana) aliweka ahadi na akaiita Agano.  Yeye Bwana ndiye alijitoa kuridhia agano hilo la kudumu na ya kwamba wataitwa ni Taifa Takatifu, ikiwa wataitii sauti yake Mungu na kutenda kulingana na amri zake (Kut. 19:5 - 6). Lakini kama ilivyo kwa mzazi (kwa familia zetu za Kiafrika), mwana umpendaye unamrudi kwa adhabu, pengine kumchapa fimbo nk. Waisareli walipomwasi Mungu kwa kutenda dhambi na machukizo, yeye Bwana aliwaadhibu kwa kuwahamisha toka nchi ya Ahadi (Kaanani) waliyopewa bure na kutumikishwa ugenini.  Walikwenda Misri wakakaa utumwani hadi Bwana alipowahurumia alipoona mateso yao akakumbuka agano lake.  Kwa mara nyingine walipofanya dhambi na machukizo, Bwana aliruhusu wakapelekwa kuwa mateka katika Babeli ya Wakaldayo kama tunavyoweza kusoma zaidi toka kitabu cha mabo ya Nyakati.

 

Ezra na Nehemia wanajitokeza zaidi wakati Wayahudi wako uhamishoni.  Wote hao waliruhusiwa kurudi Yerusalemu ili kulitengeneza upya, hekalu na kukarabati mji wa Yerusalemu vilivyoharibiwa na maadui walipotekwa na kupelekwa Babeli.  Mambo hayo yalitokea miaka 50 baada ya uhamisho 538 KK. Bila shaka yasingewezekana hayo isipokuwa tu ni huruma na ridhaa ya Mungu.  Bwana alimwinua Koreshi mfalme wa Uajemi aliyewashinda wengi na kushinda himaya Babeli.  Huyu Koreshi (mtaifa) aliguswa akaona haja ya kujenga nyumba (hekalu) la Ibada kwa Mungu wa Israeli, ambaye hata Koreshi mtu asiye mwisraeli au Myahudi, ameweza kumkiri ya kuwa huyo ndiye Mungu wa kweli (Ezra 1: 1 - 4).  Kwa hakika ni kipindi cha uamsho mpya kwa taifa teule, kwani walipata kutambua tena Agano lao na Bwana wakatubu wakapata nafasi ya kurejea Yerusalemu na kujenga upya hekalu, mji, na utaifa wao ukashika nguvu na kasi mpya tena.

Sisi wakristo leo ni Taifa teule, tena  ni watu wa milki ya Mungu, tumeitwa na tumetumiwa kwa watu na mataifa yote, tukielekeza nguvu, ari na kasi mpya kwa wale wote  ambao hawajapata nafasi ya kusikia habari njema (Injili) ya Yesu Kristo. (Ipet. 2:9).  Sisi wakristo wote ni makuhani walioteuliwa na kusimikwa tangu siku ile ya ubatizo, baada ya kumkiri Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi.  Tumeitwa tuondoke, tuenende kutangaza fadhili zake (Habari Njema za Yesu Kristo) ili wengine wapate nafasi ya kusikia Roho Mtakatifu awaongoze kukata shuri.  Matokeo ni wazi wapo watakaotii na kuamua kumfuata Yesu Kristo.  Lakini pia wako watakaosita kwanza, kwa mujibu wa mila zao, kama tnavyoshuhudia mfano kwa ndugu zetu Wamasai ( wanaishi Afrika Mashariki).  Kwa taarifa ya wainjilisti wengi  Wamasai wanaridhia, awali wanawake na watoto waingie Ukristo, (kwani makundi hayo hayatoi changamoto itakayoathiri sana mila na mshikamano wao kama jamii) endapo hao  watajiunga na ukristo.  Hata hivyo tunamshukuru Mungu kwani kwa Mungu wote wanayo thamani sawa.  Huo ni mwanzo mzuri.  Nilipokuwa mtoto hapa Uchagani, baadhi ya wanaume walikuwa bado kubatizwa lakini wake zao wakawa wakristo.  Watoto nao walifuatana na mama zao. Miaka 47 sasa baadae wote  wamekwisha batizwa wamempokea Yesu Kristo.  Kwa pamoja sasa mume, mke na watoto wanajenga Kanisa la Bwana na huo ni ushindi mkubwa wa missioni ya Kanisa, wenye mipango mizuri yenye tija.  Bwana Yesu asifiwe!

III. ONDOKA UKATENDE MAANA INAKUHUSU WEWE

Tunaporejea Neh. 2:17 - 18 tunaona Nehemia akichukuwa hatua muhimu ya kijasiri kwani alijua anahusika kama mmoja wa wajenzi kwanza Hanani (nduguye Nehemia) alimjia na taarifa za kuhuzunisha kuhusu watu waliosalia Yuda na kuharibika kiasi kikubwa mji mtakatifu wa Yerusalemu (Neh. 1:1ff).  Nehemia akifanya kazi ya kupokea wageni nakuwatunza pamoja na mfalme hasa kuwaandalia vinywaji (mhudumu nyumbani kwa mfalme), akakumbuka agano la Mungu, akaomboleza, akaom ba mchana na usiku, akatubu na kuungama dhambi za Taifa (wana) Isaraeli.  Nehemia alipoonekana hana raha mbele ya Mfalme, Mungu alikwisha mtayarisha kwenda kutenda kwa ajili ya taifa.  Alipata kibali alipomwomba Mfalme wa Uajemi akamruhusu kwenda kujenga upya mji wa Yerusalem na kurudisha hadhi yake na Taifa lile teule lenye hekalu ndani ya Yerusalemu.  Ujumbe ni kuwa mtumishi wa Mungu ndani ya makao ya mfalme Artashasta alipata neema ya kurudisha upya utaifa na nafasi yao akawaamsha tena Wayahudi kwa ari ya kumcha Mungu na kupenda kumtumikia.  Sisi Wakristo tunayo ya kujifunza toka Nehemia . Tuangalie Kanisa na nyumba zetu ziwe  mahali panapofaa kulikalisha jina la Bwana.

 

Kanisa la kwanzi ni pale nyumbani petu pamoja na jumuiya zetu ndogo ndogo siku hizi zinasaidiana, kuimarishana kiroho na kimwili. Watu wanasaidiana hasa hapa Afrika Mashariki kupitia ujirani.  Sharika ni mitaa yetu ya makanisa imejengwa na washairika wenyewe kwa moyo wa kujitegemea kwa kujitolea kutumia vizuri karama mbalimbali tulizopewa na Mungu wetu.  Tunajenga Kanisa la hapa Afrika kwa kutumia mali na rasilimali inayotoka ndani mwetu, na hii ni pamoja na Ibada zinazowakilisha wafrika pia kuwa mchango katika kanisa la  ulimwengu wote, na mahali pote.  Ona jinsi ambavyo ibada zetu zinaendelea kukua siku hadi siku. Ona mageuzi yanayotokea katika mfumo wa Uimbaji siku hizi. Ni pamoja na matumizi ya ngoma, vigelegele, makofi na kuchezesha mwili katika Ibada zetu.  Katika hali hii ya mchakato wa mageuzi ya mfumo wa Ibada, tunahitaji msaada wa Roho Mtakatifu na roho ya unyenyekevu katika kusoma na kupima tuweze kupata yale mazuri yanayoimarisha Ibada zetu na kukuza imani na uchaji wa KKKT na makanisa yote kumwinua Kristo, Afrika na ulimwenguni  pote.

IV. MWISHO

Siku ya leo ni kubwa na ya kukumbukwa kwani KKKT, (Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania) ambalo ni mwanachama muhimu wa JKT (Jumuia ya Kikristo/Baraza la KikristoTanzania) imemaliza miaka 44 tangu lizaliwe mwaka 1963.  Huu ni umri wa mtu mzima, na kwa kawaida ya mazingira ya Kiafrika, mtu mwenye familia ( watoto na hata wajukuu wadogo).  Ni kabla hata Tanganyika yenyewe kuungana na Zanzibar, kwa roho ya dhana. Umoja ni nguvu;  utengano ni udhaifu.  Yesu ametoa Agizo la kazi ya missioni na Kanisa limethibitisha utume wake kuwa chumvi na nuru ya ulimwengu.  Yapo mambo mengi yaliyofanywa na yanaendelea kutendwa na Kanisa kwa ujumla, kuonyesha mwangazo wa nuru ya Kristo, katika Elimu, Afya na Huduma za Jamii.  Sote tunamshukuru Mungu kwa yote hayo maana pasipo Yesu hatuwezi lolote sisi wenyewe. Hata hivyo yapo mapungufu pia yamesikika na kuonekana, mf. Migogoro ndani ya Dayosisi kadhaa na sharika za KKKT yenyewe na pale waliposhindwa kupata mkuu mpya (Mchungaji wa Kanisa) katika uchaguzi 2006.

Hatuna budi kutubu dhambi hii na kuwa na roho ya dhati ya kupenda kuondoa tofauti zote ili Bwana aturidhie tena Agano lake, tuanze upya na nguvu mpya na ari mpya tukisaidiwa na moto wa Roho Mtakatifu.  Nehemia aliposikia hali ngumu ya Yerusalemu Uyahudi na taifa lote kwa waliobaki pasipo kwenda uhamishoni Babeli, alilia na kusikitika.  Aliwapenda watu wake, dini yake, hekalu na taifa lake na kusikitikia nguzo muhimu zilipotikiswa na kubomoka.  Sisi wana Kanisa la Kristo, Tanzania na Afrika tuone uchungu pale misingi bora ya imani, uongozi na maadili inapotikiswa na kumomonyoka sababu ya roho ya ubinafsi.  Tuombe Mungu kama Nehemia na kumrudia mfalme Yesu Kristo ambaye ndiye atuwezeshaye, kututumia sisi kulijenga Kanisa lake, sawa na alivyomwambia Petro Mtume, "... na juu ya mwamba huu nitalijenga Kanisa langu." (Mt. 16:18).  Tumwombe Bwana atuchagulie mtu kiongozi (Mkuu wa Kanisa) atakayekuwa Mchungaji wa Kanisa. AMEN!

 

 

 

 

 

 

 Rev Mch Dawson E Chao
SLP 3050 MOSHI
E-Mail: dawsonchao@yahoo.com

(zurück zum Seitenanfang)