Göttinger Predigten

Choose your language:
deutsch English español
português dansk

Startseite

Aktuelle Predigten

Archiv

Besondere Gelegenheiten

Suche

Links

Konzeption

Unsere Autoren weltweit

Kontakt
ISSN 2195-3171





Göttinger Predigten im Internet hg. von U. Nembach

The Fourth Sunday in Lent, 18.03.2007

Predigt zu Matthäus 14:13-21, verfasst von Sifuel Macha

Mpendwa Msomaji, Bwana wetu Yesu Asifiwe. Somo letu kwa siku ya leo linatoka katika Injili kama alivyoandika Mwinjilisti Mathayo 14:13 - 21.

Naye Yesu aliposikia hayo, aliondoka huko katika chombo, akaenda mahali pasipo watu, faraghani. Na makutano waliposikia walimfuata kwa miguu kutoka mijini mwao. Yesu akatoka, akaona mkutano mkuu, akawahurumia akawaponya wagonjwa wao. Hata kulipokuwa jioni, wanafunzi wake walimwendea, wakasema, Mahali hapa ni nyika tupu, na saa imekwisha pita; uwaage makutano, waende zao vijijini, wakajinunulie vyakula. Yesu akawaambia, Hawana haja kwenda zao, wapeni ninyi kula. Wakamwambia, hatuna kitu hapa ila mikate mitano na samaki wawili. Akasema, nileteeni hapa. Akawaagiza makutano waketi katika majani; akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni akabariki akaimegaile mikate akawapa wanafunzi, wanafunzi wakawapa makutano. Wakala wote wakashiba, wakayaokota masazo ya vipande vya mikate, vikapu kumi na viwili, vimejaa. Nao walikula walikuwa wanaume wapata elfu tano, bila wanawake na watoto.(Mathayo 14:13 - 21)

Tuombe

Tunakushukuru Mwenyenzi Mungu kwa kutupa tena siku ya leo. Asante Bwana kwa kuwa unaangalia ulimwengu wote kwa huruma yako. Asante kwa kuwa unatulisha kwa mkono wako wenye nguvu. Tunakuomba wabariki wale wote wanaowalisha wengine. Tupe ee Baba kibali cha kupata ule mkate wa mbinguni katika uzima ule wa milele. Amina.

1. Bwana Yesu huwajali wenye shida za mwili, njaa na magonjwa.

Mpendwa msomaji, katika somo tulilolisoma zipo hoja kadhaa za msingi za kufahamu

kabla ya kuendelea, nazo ni mbili.

(i) Hoja ya kwanza ni ule mvuto wa Bwana Yesu kwa watu wenye shida kuliko mpango wake wa shughuli. Kwa mujibu wa uandishi wa Mathayo katika sura ya (14:12) Bwana Yesu anapata taarifa mbaya za kuuawa na kuzikwa kwa Yohana mbatizaji, mauaji yaliyofanywa na Herode katika ahadi yake ya kumfurahisha bintiye, bila shaka na mke wake. Bwana Yesu anaondoka chomboni na kutafuta faragha kama mwanadamu apate kumwombelezea Yohana, kumbe mwana wa Adamu hana mahali pa kuulaza ubavu. Hana faragha hana mahali ambapo watu wenye shida hawatamfikia.

(ii) Hoja ya pili ni juu ya kilio cha Yohana kabla ya kifo alipokuwa gerezani. Yawezekana kuwa Yesu alishtushwa na kifo cha Yohana maana Yohana alishatuma ombi kwamba mbona ameachwa gerezani ili hali Bwana Yesu alikuwa na uwezo wa kumwondoa? Bwana Yesu hakutarajia Yohana angalikufa mapema hivyo maana alimwambia nguvu za Mungu zinatenda miujiza mikubwa kama vile vipofu kuona na viwete kutembea, sembuse kumtoa yeye gerezani?

2. Umati Uliomfuata Yesu Umepata Shida ya Njaa

Yaonekana kuwa watu hawakutarajia huduma ingalichukua muda mrefu, vinginevyo

wangalibeba chakula. Hitaji la chakula nalo linamgusa Bwana Yesu hadi kutaka

afahamu kama wanafunzi wake walikuwa na uwezo wa kuwalisha watu. Kwa

vyovyote vile hapakuwepo na uwezo maana watu walikuwa wengi. Hali hii imetokea

ili Mungu apate kudhihirika akitenda miujiza.

MUNGU ANAWALISHA WATU WANAPOTINDIKIWA

(a) Maandiko Matakatifu katika (2 Falm. 4:42) yanatuonyesha nia ya Mungu ya kuwalisha watu hasa pale ambapo imani ya mwanadamu inapoyumba. Nabii Elisha aliwaandalia watu chakula maana Bwana anasema "... uwape watu ili wale kwa kuwa Bwana asema hivi "watakula na kusaza". (2falm. 4:42).

(b) Maandiko pia yanatuonyesha Mungu akitenda miujiza katika akiba ya yule mwanamke wa Sarepta si kwa katika kutenda tu miujiza bali kwa kuwa imani imedhihirika mama wa Sarepta aliamini na mwujiza wa chupa kutopungua mafuta wala pipa kutopungukiwa unga. Kumbe Mungu hupenda kufanya kazi pamoja na wanadamu. Utayari wa mwanadamu umefanya huduma kuwa nyepesi. (I falm. 17: 9 - 16). Kumbe Bwana yuko tayari kutusaidia katika shida zetu ili mradi tu tuwe tayari kuonyesha kuwa tutampa ushirikiano na kwamba tunahamu ya kuondokana na shida zetu.

3. CHAKULA NA MASAZO ISHARA KUU KWA WENYE NJAA

Mpendwa msikilizaji, hatuoni ulinganifu kati ya vianzo vya chakula - samaki na mkate na makapu 12 ya masazo baada ya watu kushiba. Kwa kuwa idadi ya wanafunzi ilikuwa 12 na makapu ya masazo 12 msomaji atavutwa kusimuliwa kuwa pengine pana siri ya ki-masihi katika lishe hii. Kwamba wanafunzi wachukue nafasi yao kila mmoja katika kuwatunza wenye njaa maana masihi yupo atatenda kama alivyotenda.

Mpendwa msomaji, dunia kwa sasa ipo katika uhitaji mkubwa sana wa chakula. Yasemekana ¹/3 theluthi moja ya watu hupata mlo mmoja tu kwa siku duniani. Kuongezeka kwa matokeo ya vita katika ukimbizi kunafanya idadi ya wenye njaa kuongezeka. Kwa sasa zaidi ya asilimia 2 (2/100) ya wakazi wa dunia wako ukimbizini, ama ndani au nje ya nchi zao. Hawa wana njaa na ni wajibu wetu kuwatunza.

Wakati hawa wenye njaa wakitaabika, bado tunasikitishwa na wachache wanaotumia chakula vibaya. Watu wametumia nafaka kutengeneza pombe badala ya chakula. Na baadhi wamekuwa wakimwaga chakula ili hali mamia wanateseka.

4. BWANA YESU ANACHOCHEA UFAHAMU KUWA YEYE MWENYEWE NI ZAIDI YA CHAKULA CHA SASA

Ndugu msomaji, Bwana Yesu anajua fika kuwa watu tunakula ili tuishi na baadaye tufe maana tulizaliwa. Bwana Yesu anatutaka mimi na wewe tupate hamu ya chakula cha uzima wa milele, ambacho ni Yesu mwenyewe. Kuwa na hamu na Yesu ni kutenda sawa sawa na mapenzi yake. Hatutaweza kufanya hivyo kama tuko nje ya Kristo. Kuwa ndani yake kunatufanya tuwe watu wa kukua kila mara maana kwake kuna uwezo (Yn. 1:12, 13).

5. KULISHWA WATU KAMA NJIA YA UINJILISTI

Ushuhuda kutoka kwa wenye njaa unasema "nalikuwa na njaa mkanipa chakula". Yeye aliyekuwa na njaa apatapo msaada wa chakula, anao ujumbe. Hayati Baba Askofu Josia Kibisa wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Magharibi alinukuu maneno ya mwalimu wake akisema "Ili upate kumsimulia mtu habari za wokovu (salvation) ni budi utangulize mambo mawili kwanza:

1. Supu - Mwenye njaa hawezi kuwa msikilizaji pasipo kushiba.

2. Soap (sabuni) Aliyekula apate sasa sabuni ili aondoe na vumbi, uchafu na macho

yaone, masikio yasikie. Sasa waweza kumsimulia habari za

wokovu (salvation) na akakusikia maana ameona supu na sabuni

ikimtoa mbali.

Mpendwa msomaji Bwana Yesu anakuita ili uwe mhubiri kwamba Yesu anaokoa. Lakini kabla hawajahusikiliza wanahitaji chakula na sabuni. Tunamshukuru sana Mungu kwa mashirika kama WFP (World Food Program) na Bread for the World (Mkate kwa Ulimwengu) ambayo mara zote yapo tayari kuwanusuru wenye shida. Sijui kama umewahi kujiuliza kuwa wanapata wapi fedha? Jibu ni kuwa wamepata changizo na msaada toka kwa watu wema. Sijui wewe uu mwema au mbaya. Bwana Yesu anakupanga nyuma ya makapu 12 sambamba na mitume ili uchangie japo kidogo, naye atende mwujiza. Je utatoa samaki wangapi, au mikate mingapi. Bwana akubariki. Amen.



Sifuel Macha
Chuo cha Biblia na Theologia Mwika,
S.L.P 3050,
MOSHI.

E-Mail: mwika@elct.org

(zurück zum Seitenanfang)