Göttinger Predigten

Choose your language:
deutsch English español
português dansk

Startseite

Aktuelle Predigten

Archiv

Besondere Gelegenheiten

Suche

Links

Konzeption

Unsere Autoren weltweit

Kontakt
ISSN 2195-3171





Göttinger Predigten im Internet hg. von U. Nembach

MAHUBIRI: JUMAPILI ? SIKU YA BWANA YA KWANZA BAADA YA UTATU TAREHE, 10.06.2007

Predigt zu Lukas 16:19-31, verfasst von Johann W. Kaale

Utangulizi: Tokea mwanzo wa Injili, Mwinjilisti Luka alionya na kutahadharisha ni mambo gani yanayoweza kuhatarisha maisha yetu ya Kikirsto.  Mwinjilisti Luka alidhihirisha kwamba kupenda mali na utajiri wa dunia ni chanzo kitakachowanyima wengi ule ufalme wa mbinguni.  Tangu mwanzo wa Injili shetani alijitokeza akimwonyesha Bwana wetu Yesu Kristo falme zote za dunia akamwambia, " Nitakupa wewe enzi hii yote, na fahari yake, kwa kuwa imo mikononi mwangu, nami humpa yeyote kama nipendavyo.  Basi wewe ukisujudu mbele yangu yote yatakuwa yako".

 (Lk. 4:6 - 7).  Lakini Yesu Kristo alimjibu shetani akamwambia, "Imeandikwa, msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake." (4:8)

Maneno hayo ya Mwinjilisti Luka yanathibitishwa zaidi katika somo la leo katika sura hii ya 16: 19 - 31 kwa mfano huu wa Tajiri na Lazaro maskini.  Hamu ya kujilimbikizia mali nyingi na uchoyo wake huyu tajiri zimemtia katika mateso ya kuzimu ambako Abrahamu wala Lazaro hawawezi kumsaidia na kumwokoa.  Uchoyo wake ulimfanya kuwa mtumwa wa "Mungu Mali"." Tajiri huyu alipaswa kutambua kwamba si rahisi mwanadamu kumtumikia Mungu na mali kwa wakati mmoja. (16:13). Wako baadhi ya watu wenye kupenda sana kusikiliza Neno la Mungu kwa imani, lakini polepole huvutwa na hamu ya kupata mali na  anasa za maisha ya dunia na hatimaye huipoteza imani hiyo na hata wokovu wao.  Ndivyo hata ule mfano wa mkulima aliyesia mbegu shambani, nyingine zikaanguka kati ya miiba, na ile miiba ilipoota ikazisonga, unavyotufundisha. (8:14).  Kadhalika siku moja mtu mmoja tajiri alimjia Yesu kupata ushauri ni kwa jinsi gani angeliweza kupata uzima wa milele.  Yesu Kristo alimshauri auze mali yake yote awagawie maskini.  Mtu huyo aliposikia hivyo alihuzunika sana kwa maana alikuwa na mali nyingi.  Yesu alipoona vile, kwa masikitiko alisema. "kwa jinsi gani ilivyo vigumu kwa matajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.  Ni vyepesi ngamia kupita katika tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu. (18:18 - 25).

Swali: Ni kwa nini utajiri mara nyingine unajulikama kama "mali dhalimu?"(16:9).  Hakika baadhi ya watu matajri duniani sasa hivi wamejipatia au wanajipatia mali kwa njia ya wizi na ujambazi, udanganyifu na utapeli, rushwa na dhuluma.  Watoto wengi wamekwisha poteza wazazi wao duniani kutokana na vifo vya ugonjwa wa UKIMWI (HIV - AIDS). Baadhi ya wazazi hao walikuwa ni watu "wazito" kifedha na hata kwa kumiliki mali nyingi.  Sasa hivi imetokea kwa baadhi ya watoto hao yatima walioachwa na wazazi matajiri kudhulumiwa fedha na mali hiyo na walezi wao; wengi wao wakiwa ni ndugu wa marehemu wahusika.  Mali yote ni lazima itumike kwa ajili ya wahitaji na wenye shida mbalimbali.  Kulimbikiza mali tu na kuiweka bila kusaidia wengine ni kuwanyima wengine riziki na kuzuia maondeleo yao; hivyo nI dhambi na inahitaji toba.

Zakayo, yule mtoza ushuru, alimwelewa vizuri Yesu akitaka Yesu mwenyewe awe rafiki yake akasema, "Bwana, tazama, nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimemyang'anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne." Yesu alimjibu akamwambia "Leo wokovu umefika nyumbani humu." (19:8.9).  Kugawa mali kwa maskini na wahitaji wengine si swala la hiari bali ni agizo au amri. "Uza kila ulicho nacho, ukawagawie maskini, na hivyo utakuwa na hazina yako mbinguni, kIsha njoo, unifuate." (18:22)

Yohana Mbatizaji naye aliwaasa watu waliomjia wajifunze yatakayowapasa kufanya.

" Aliye na nguo mbili amgawie yule asiye na nguo, aliye na chakula afanye vivyo hivyo." Nao watoza ushuru wakaonywa wasitoze zaidi ya kima kilichowekwa na serikali, na maaskari wakatahadharishwa wasichukue vitu vya watu kwa nguvu wala kumshtaki mtu ye yote kwa uwongo; bali watosheke na mishahara yao. (3:10 - 14).  Yesu aliwahoji wanafuzi wake akisema, "Mtu atakuwa na faida gani kwa kuupata utajiri wa dunia nzima akijipoteza au kujiangamiza mwenyewe?" (9:25).  Hakika, nafsi zetu na roho zetu zina thamani kubwa sana kuliko fedha na vitu vingine vyote.  Hapa Bwana wetu Yesu Kristo hana nia ya kutufundisha elimu ya sheria ya siasa na uchumi, wala kuhusu maadili, bali anataka tutambue tofauti iliyopo kati ya sheria na haki.  Kwa jinsi hiyo tujifunze vizuri jinsi ya kuthamini nafsi na roho zetu zaidi kuliko fedha na mali tutafute kwanza ile "hazina ya mbinguni" au "uzima wa milele" tulioahidiwa naye Bwana wetu Yesu Kristo.

Je, nani atakayeingia katika uzima huo wa milele?  "Yeyote aliye mwaminifu katika mambo madogo, yaani mwenye kumiliki na kutumia mali ya dunia kwa haki na usawa; yeye aliye mtumishi mwaminifu ambaye atawatumikia wengine kwa hekima na imani na kumpatia kila mmoja yanayomstahili."  "Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiwa ...kwa kuwa kipimo kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa."       (6: 38). Mwenye kugawa mali kwa kuwasaidia wenye shida na wahitaji, hupamba roho yake ukarimu na kila fadhila, maana hujijengea utu wema, naye ameahidiwa uzima wa milele.

Katika Biblia umaskini umepewa sifa kuu kwa sababu huzaa na kudhihirisha hazina ya kiroho.  "Heri ninyi mlio maskini, kwa sababu ufalme wa mbinguni ni wenu." (6:20).  Yesu mwenyewe alikiri kwamba hakuwa na mahali pa kupumzikia (9:58); na hata alipowaita wanafunzi wake "waliacha vyote" wakamfuata (5:11).  Yesu Kristo amemweka mbele yetu Lazaro maskini kuwa mfano wa mtu mwema aliyevumilia mateso yote hata Mungu mwenyewe alipompokea juu mbinguni kwa faraja ya milele.  Wale walio na umaskini kama huu kwa ajili ya Kristo hawana haja ya kuwa na wasiwasi wala mahangaiko kwa kuwa tumaini lao na kimbilio lao ni Mungu Baba Mwenyenzi.  " Msiogope, enyi kundi dogo, kwa kuwa Baba yenu amependa kuwapeni huo ufalme.  Viuzeni mlivyo navyo, mtoe sadaka.  Jifanyieni mifuko isiyochakaa, na jiwekeeni hazina mbinguni ambako haitapungua.  Huko wezi hawakaribii wala nondo hawaharibu.  Kwa kuwa hazina yenu ilipo ndipo, itakapokuwa na mioyo yenu." (12: 31 - 34).

Bwana Mungu alibariki Neno lake; abariki pia katika kuingia na kutoka kwetu. Amen!



Johann W. Kaale
Moshi ? Tanzania
E-Mail: Rev.kaalejohann@yahoo.com

(zurück zum Seitenanfang)