Göttinger Predigten

Choose your language:
deutsch English español
português dansk

Startseite

Aktuelle Predigten

Archiv

Besondere Gelegenheiten

Suche

Links

Konzeption

Unsere Autoren weltweit

Kontakt
ISSN 2195-3171





Göttinger Predigten im Internet hg. von U. Nembach

SUNDAY FIRST JULY, 2007, 15.07.2007

Predigt zu MATHAYO 5:43 - 48, verfasst von Amini A. Njau,

  

SIKU YA BWANA YA 6 BAADA YA UTATU

KICHWA:  AMRI YA UPENDO

SOMO:  MATHAYO 5:43-48

•1.                  UTANGULIZI:

 Somo hili ni sehemu ya Hotuba ya Yesu Kristo kwa makutnao waliomfuata ili kusikiliza mafundisho yake.  Yesu aliona vyema kupata mazingira mazuri ili watu wote waweze kumsikia, ndipo alipopanda juu ya kilima, (Mathayo anasema mlimani Math. 5:1) wanafunzi na wafuasi wake walimfuata.  Yesu alifungua kinywa chake na kuwafundisha mambo mengi.

 Yesu alikuwa mwalimu mzuri na aliyefundisha kwa kutumia mifano dhahiri ili wasikilizaji wake waelewe.  Aliwafundisha mambo mengi yaliyotendeka kati yao na kwa kanuni za mila zao, ambayo hayakuonyesha mapenzi ya Mungu; hayakuonyesha kutendeana haki wala huruma.  Hivyo katika hotuba yake pale mlimani kama inavyoonekana katika Mathayo 5:7; aliwafundisha makutano kwa ujasiri na kwa mamlaka, hata waliomsikiliza walishangaa kwa jinsi alivyofundisha, kama mtu mwenye amri, wala si kama Wandishi wao.  (Mathayo 7:28-29).

•2.                  YESU ALIFUNDISHA JUU YA UPENDO:

Katika hotuba ya Yesu pale mlimani, sehemu moja ya mafundisho yake ilikuwa juu ya "UPENDO".  Kumpenda jirani kama nafsi yako, ni sehemu ya pili ya ile amri kuu: (Marko 12:30-31).

Yesu alizungumza haya kwa wale makutano kwa jinsi alivyoona waliishi bila upendo. Wayahudi hawakuwapenda Wasamaria, wala Wayunani, hawakuchangamana, na aidha wao wenyewe kwa wenyewe walifarakana bila upendo; kumbuka makundi (Sects) yao:  Mafarisayo, Masadukayo; Waandishi, Watu wa kawaida na Wamataifa.  Ubaguzi ulikuwa mkubwa.

Yesu alipozungumza juu ya kumpenda jirani alikuwa na maana ya watu wote, walioumbwa na Mungu kwa mfano wa Mungu mwenyewe ni jirani zetu; weupe, weusi, wakubwa, wadogo, maskini, fukara, wa jinsia zote na wa mataifa yote ni jirani.

Yesu aliagiza kuwapenda maadui na kuwatendea mema, siyo baya kwa baya au ovu kwa ovu, haya hayakuwa mageni kwao, kwa sababu yako katika sheria walizopewa na Mungu kupitia Musa. (Walawi 19:17-18).

 Aidha mwandishi anaonyesha kwamba, Yesu anafundisha kuwapenda wote hata wale wanaolichukia na kulitesa Kanisa.  Hao nao waonyeshwe upendo, wavutwe kuja kwa Yesu kwenye kundi moja na Mchungaji mmoja Yesu Kristo. (Yoh. 10:16)

Yesu mwenyewe alifundisha juu ya upendo na yeye mweneywe akiwa kielelezo.  Yeye aliwapenda watu wote wa umri mbalimbali na wa jinsia mbalimbali na wa vipato na uwezo mbalimbali.

Katika maandiko Matakatifu tuna habari za Yesu kukutana na watoto, kuwakaribisha kwake na kuwabarikia, (Mariko 10:13-16).

Yule mwanamke Msamaria, Yoh. 4:7ff.

Yesu nyumbani kwa Zakayo, Lk 19:1ff

Yesu aliwaponya wagonjwa ... n.k.

Yesu alionyesha upendo kwa watu wote na kuwatendea haki pia kuwahurumia.  

•3.                  UPENDO KATIKA MAZINGIRA YA LEO:

Upendo umepoa kati ya jamii ya leo kiasi ambacho binadamu anatisha kuliko kukutana na mnyama wa porini, simba au chui.

Watu hawatendeani haki wala hawana huruma kwa wengine, watu wamefikia hatua ya kuuana kwa silaha kali (Sophisticated weapons).  Aidha watu wanahudhuria mafunzo ya hali ya juu kwa gharama kubwa, kutengeneza silaha kali, kwa gharama kubwa, viwanda vikubwa vya kutengeneza silaha - vyote hivyo ni kwa ajili ya kumwangamiza mwanadamu.  Ni kukosekana kwa upendo.

Ndugu wanakosana, wanapigana, wanaendeana kwa waganga ili kuangamizana, ni kukosekana kwa upendo.

Jamii inafarakana na kupigana (civil war) ni kukosekana kwa upendo, hata nchi na nchi zinapigana, watu wanauawa, wasio na hatia, watoto, kina mama, wazee n.k.   Ni kukosekana kwa upendo.

Baadhi ya mataifa yenye nguvu za kiuchumi yanayatisha mataifa maskini - mataifa machanga yanaishi kwa makombo ya mataifa yenye nguvu kiuchumi.  Ni kukosekana kwa upendo.

Jambo la kusikitisha zaidi ni pale watu binafsi kwa kutumia nafasi zao za madaraka au za kiuchumi, kuwanyima haki zao, kutowaonea huruma. Hata kule kupanga viwango vya mapato, mishahara, maslahi kunaonyesha bayana jinsi wachache wanavyojineemesha kwa jasho la walio wengi. Ni kutokuwa na upendo.

  4.       MFANO:

Mama mmoja alikuwa na watoto wake wawili wadogo. Mama huyu alikuwa na  nafasi nzuri kiuchumi, alikuwa na nyumba nzuri na aliwekewa wigo{fense}

 na lango zuri la kuingia.

Siku  moja mama huyu alikwenda shambani, akawaacha hao watoto wawili nyumbani; hao watoto walizoea kucheza na watoto wengine wawili wa jirani, lakini wazazi wao walikuwa maskini {fukara} na mara nyingi hawakupata chakula vizuri.

Mama huyu mwenye uwezo alizoea kuwa na mikate ndani ya kabati yake na wale watoto wake waliozoea kunyofoa kiini cha mkate na kula, na kula; walipoulizwa walikataa. Huyu mama aliona kwamba wale watoto wa jirani ndio wanaokula mkate wake. Alichukua sumu ya panya na kuiweka ndani ya mkate, huku akiwa amewapa watoto wake chakula cha kutosha. Lengo la huyu mama ni kuwakomoa au kuwaadhibu watoto wa jirani aliodhani kuwa wao ndio hula mkate wake kabatini.

Mama aliondoka kwenda shamba kumbe watoto wake mwenyewe waliendelea na ile tabia ya kunyofoa mkate, walipokula matumbo yaliwauma sana, Walilia kwa sauti kubwa.

Yule mamaa mnyonge wa jirani alisikia kilio cha hao watoto akawakimbilia, aliwakuta wakigaragara chinni kwa maumivu. Huyu mama aliwakimbiza hospitalini na huko daktari aliwatapisha na kusema walikula chakula chenye sumu. Walipopata nafuu aliwarudisha nyumbani na wakati huo mama yao alikuwa amerudi kutoka shambani. Bila shaka huyu mama alitambua kosa lake. Yaliyoendelea wanayajua.

Je, Yule mama tajiri alionyesha upendo kwa watoto wa jirani yake? Je mama maskini alioonyesha chuki kwa watoto  wa jirani yake.?

Mara nyingi watu wenye nafasi, mali, vyeo, madaraka, hawaonyeshi upendo na huruma kwa wanyonge.

Yesu anatukumbusha kuwa na upendo kwa jirani zetu kama yeye alivyotupenda tangu mwanzo. (Yoh.13:34-35)

NB. Mara nyingi Mungu hupenda kumsaidia mtu wake kupitia kwa mtu mwingine _ jirani yumkini Mungu amepitisha msaada wa jirani yako kwako, kwa kukuongezea neema ya mali, fedha, dhamana fulani fulani n.k ili kupitia kwako, neema hiyo imfikie mja wake ambaye ni jirani yako. Je! utatambua hilo-Roho Mtakatifu akufunulie.

 

 

 

 

 



Pastor Amini A. Njau,
Evangelical Lutheran Church in Tanzania
Mwika Theological College of Tumaini University

E-Mail: amininjau @ yahoo.com

(zurück zum Seitenanfang)