Göttinger Predigten

Choose your language:
deutsch English español
português dansk

Startseite

Aktuelle Predigten

Archiv

Besondere Gelegenheiten

Suche

Links

Konzeption

Unsere Autoren weltweit

Kontakt
ISSN 2195-3171





Göttinger Predigten im Internet hg. von U. Nembach

MAHUBIRI YA JUMAPILI TAREHE, 05.08.2007

Predigt zu Luca 10:38-42, verfasst von Mch. John A Moshi.

                                   

Utangulizi: Wakati mwingine tumesahau kwamba tupo duniani ili tumjue Mungu na maajabu yake. Tukafikiri tuna haki ya kuwepo duniani, na hivyo tukajifanyia mambo yetu wenyewe. Hata Mungu  mwenye haki zote akasahaulika na kukosa nafasi katikati ya viumbe wake aliowaumba kwa nguvu na kwa mfano wake

                  Somo tulilosoma kutoka injili ya Luka linatuonyesha akina dada wawili waliotamani kukaa na Yesu. Hili lilitokea baada ya Yesu kukaribishwa nyumbani kwa dada hawa wawili. Hapana shaka walifurahia sana kuwa na Yesu nyumbani kwao. Ni kawaida mgeni maarufu anapofika nyumbani kuandaliwa na kupokelewa kwa heshima zinazostahili. Tunaona Mariamu umbu lake Martha ameamua kukaa na Yesu kwa kufanya mazungumzo naye wakati Martha mwenyewe anahangaika kuandaa chakula jikoni. Tunaambiwa, "Lakini Martha alikuwa akihangaika kwa utumishi mwingi" mst. wa 40. Pengine Martha alifikiri kumtunza mgeni kwa chakula na kumuonyesha ukarimu fulani, ingekuwa furaha kubwa kwa mgeni! Na hili ni jambo la kibiblia. Ni mawazo mazuri ambayo wengi wetu tunayazingatia pindi tunapopata mgeni. Lakini Mariamu aliwaza nini. Yeye alitaka akae naye azungumze naye amsikilize, au labda alihitaji ushauri kuhusu jambo lake Fulani ambalo lilikuwa likimsumbua au amuangalie tu Yesu ambaye alikuwa maarufu sana huko uyahudi. Au Mariamu aliona kwa kuwa Martha yuko jikoni tayari, hakuna haja ya yeye kumsaidia bali akae na Yesu ili asijisikie mpweke. Hali hizi zote ziko katika mazingira yetu, sisi nasi tunafanya hivyo. Yaani kuhakikisha kwamba mgeni anatunzwa katika hali zote. Mgeni hawezi kuachwa peke yake sebuleni, wanakuwepo wanaozungumza na mgeni na wengine wanakimbiakimbia kumtafutia chochote ili asije akaondoka bila kupata hata maji ya kunywa. Ni utamaduni wa kiafrika kwamba mgeni anakirimiwa kwa kadiri ya uwezo wa mwenyeji.

                   Kwa mtazamo huu, sioni tatizo hapa. Shida imekuja hasa Martha alipohitaji msaada katika shughuli zake huko jikoni. Yesu ndiye aliyetakiwa kumruhusu Mariamu akamsaidie mwenzake. Majibu ya Yesu yanakuja kinyume kabisa na matazamio sio tu ya Martha bali pia mmatazamio yetu sisi waafrika. Mawazo ya Yesu ni tofauti na mawazo yetu sisi wengi. Martha anaambiwa anasumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi.

      Inaonekana Yesu Kristo alikuja kwa jambo moja tu kwa ajili yao. Alihitaji wafahamu lengo la yeye kukubali mwaliko wao. Hatuna hakika kama dada zetu hawa walimfahamu vizuri Bwana Yesu. Anamdokezea Mariamu kwa sentensi moja kwamba, "lakini kinatakiwa kitu kimoja tu". Hakuna sababu ya kuhangaika na vitu vingi hapa duniani. Martha alihitaji kuelewa kwamba Yesu alihitaji moyo wake zaidi na wala si kusubiri maandalizi ya chai au chakula. Na ndiyo maana akamwambia kwamba kunatakiwa jambo moja tu kwake. Kuacha mambo mengi ya dunia hii yanayotusonga na kumkimbilia yeye. Mambo mengi yanatufanya sio tu kumsahau yeye bali hata kumdhihaki na mwishoni kukosa nafasi ile aliyotakiwa kuwa nayo ndani ya maisha yetu.

      Jambo ambalo Yesu alilitaja pale nyumbani kwa Martha na Mariamu ni kuchagua fungu lililo jema na hivyo kumlinganisha na Mariamu aliyefanya vizuri pale alipokaa na Yesu kumsiliza, alichagua fungu lililo jema. Hili ndilo jambo moja na la muhimu la kuchagua pengine kwa watu wote wanaotaka kwenda mbinguni. Yesu ndiye mchungaji mwema kwetu na hivyo tunahitaji kumchagua yeye. Kwa hakika vitu vingi vya dunia vinatufanya tuanamsahau Mungu aliyetuumba na hivyo kufanya yale tunayofikiri kwamba ni mazuri kwa Mungu hata pasipo kumshirikisha yeye.

      Yesu anataka tumchague yeye kwani ndiyo lengo la Mungu kwamba tukimuangalia yeye aliyetumwa kwetu tupate kupona na kuokolewa. Kukaa na Yesu maana yake ni kumtegemea na kumtumikia kuliko vitu vyote. Anakuwa ndio tumaini letu. Tunapata nafasi ya kumsikiliza pale tu tunapokaa naye. Mariamu aliambiwa kuwa amechagua fungu lililo jema kwa sababu alichagua kukaa na Yesu na au ili amsikilize. Hili ndilo jambo kubwa ambalo tunatakiwa kuchagua tungali hapa duniani. Yesu pia anasema ni chakula cha uzima, anayemchagua yeye amechagua chakula cha uzima. Kukaa na Yesu kunatupa shibe ya kiroho na hata kupata amani ya mwili. Kukaa na Yesu kunatufungulia siri kubwa ya kumfahamu Mungu zaidi na hata siri ya mbinguni, na hivyo kufahamu mambo mengi ya mbinguni na uzuri wake.

Twaweza kufikiri kuhangaika sana hapa duniani ndio kujipatia nafasi ya kukaa na Yesu katika maisha hayo. Lakini Yesu anaonyesha kuwa, pamoja na ukarimu huo hatujafanya lolote kama hatujaonyesha kwa dhati nia na kupenda kukaa naye kiroho. Hapa ni lazima kutumia akili na hekima kama tunataka kweli kwenda mbinguni. Swala la kuchagua hapa lazima liwe la hekima. Pengine twaweza kujiuliza ni kwa kiasi gani tunampa Mungu nafasi katika maisha yetu ya kila siku? Pengine ni roba tu,au nusu tu!! Mungu anashirikije na sisi katika kazi zote tunazofanya kila siku, na tuna uhakika kwamba tuko naye? Ni maswali ambayo kila anayesoma maneno haya atapaswa kufikiri kwanza kabla hajajibu kutoka rohoni kwake. Lakini hekima ya kufanya haya tutatoa wapi? Mkristo anayehitaji hekima atapaswa kusoma neno la Mungu wakati wote. Hapa hata mgeni akija kwake anaweza kujua hitaji lake kwa kuzungumza naye kwanza kabla hajamhudumia. Yesu anahitaji watu wote wakae naye kwanza ili waweze kumtumikia kwa furaha.

Wapendwa tumkubali Yesu aingie ndani ya maisha yetu, tukae naye na kasha tupate baraka zake ili mwishoni mwa maisha haya tuingizwe naye mbinguni. Yesu anapoingia kwetu, anatuhitaji tukae naye. Tusome neno la Mungu ili tuweze kuelewa haya yote yatusaidie kusogea karibu zaidi na Mungu. Kukaa na Yesu ni kumkubali na kupokea wokovu aliouleta kwetu kwa njia ya kifao cha msalaba ili sisi sote tupate kuwa huru mbali na dhambi. Mwishoni ni kuingizwa katika uzima wa milele. Bwana awabariki. Amen.

 

 



Mch. John A Moshi.

E-Mail: johnmoshi@yahoo.com

(zurück zum Seitenanfang)