Göttinger Predigten

Choose your language:
deutsch English español
português dansk

Startseite

Aktuelle Predigten

Archiv

Besondere Gelegenheiten

Suche

Links

Konzeption

Unsere Autoren weltweit

Kontakt
ISSN 2195-3171





Göttinger Predigten im Internet hg. von U. Nembach

THE 15TH DAY AFTER THE TRINITY, 16.09.2007

Predigt zu Luke 12:22-31, verfasst von Peter MREMI

"

 

 

   NENO KUU: MTAFUTENI MUNGU   

 

 

 

UCHAGUZI WA BUSARA NI KUMTAFUTA MUNGU

 

 

Tunaposema   "Mtafuteni Mungu"    itaonekana kama tunakwenda kinyume na wazo kuu la somo letu hili somo linakaza kwamba  "Msisumbukie ambo lolote" maana  "hata mkisumbuka hamwezi kufanya lolote" Ni kama mtoto anayejishughulisha sana tena kwa umakini mkubwa kujenga nyumba ya ghorofa kumbe kwa kweli machoni petu anacheza tu kwa kupanga magunzi mchangani.

Kwa upande mwingine tutashangazwa sana na mtu anayetufundisha "kukaa bure". Kumbe kwa kweli haifai kukaa bure, maana huo ni uvivu, na mvivu anakemewa na Neno la Mungu.  2 Thes.3:10

Katikati ya mawazo haya mawili, Bwana Yesu anataka kutuonyesha namna ya kujishughulisha kunakokubalika, kujishughulisha  kunakokubalika, kujishughulisha kwenye baraka na kujishughulisha kwa halali.     Tunaweza kumwona mtume wa Bwana  akijumlisha mafunzo haya katika maneno,  "Mtwikeni Yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana na mambo yenu" 1 Pet. 5:7.

Katika somo letu hili la Lk.12:22 na kuendelea ,  Bwana Yesu  anatoa fundisho kutokana na Bwana fulani aliyetaka Bwana Yesu awe "Hakimu", kati yake na ndugu yake anayemdhulumu urithi -kulingana na madai yake,  labda tungetazamia Bwana Yesu angemsaidia mwonewa huyu kwa kuwa Bwana wetu ndiye,  "Mtegemezi wa wanyonge na wanaodhulumiwa".  Pengine pia ndugu huyu alipata ujasiri wa kuweka madai yake haya kwa kuwa alijua kuwa nduguye anamheshimu Bwana  Yesu.

Lakini tunaweza kujiuliza swali: Je,  kuna dhuluma ya kweli?   Mbona huduma hii haina wakili ila ni ya utetezi binafsi tu?  Je, hii haiwezi kuwa namna fulani ya unyang'anyi au ubinafsi?   Kwa haya yote hatuna jibu.

Bwana Yesu anawafahamu  ndugu wahusika wote.   Tena anaifahamu vizuri roho ya mdai.   Anajua kwa mfano,  haki ya mgawa urithi, uwezo wa kumiliki na kutumia vizuri mali iliyoachwa na mengine yote yanayohusiana na mgogoro wa mdai na nduguye. Lakini zaidi ya hayo  anaona hatari iliyo mbele ya huyo mhitaji wa mali. Hivyo anamwonya yeye, ndugu yake na wote wanaosikia waangalie ili wasije  wakawa  "Wapumbavu"   wa mali.  Lk.  12: 20.

Katika maisha ya utafutaji wa mali  kwa mwanadamu kila  mara huwa kuna jambo linalosahaulika.  Mtu hupenda kujilimbikizia - zaidi ya wengine na kumsahau mwenye  mali  muumba  wake.

 

Kwa fundisho la  mlalamikaji huyu Bwana Yesu anawawekea wanafunzi wake msingi wa  maisha bora ya utafutaji wa mali. Mkristo wa kweli awe na  Roho ya namna gani katika kutafuta mali? Nguvu nyingi kabisa ya Mkristo aiweke wapi katika hali yake ya kujitengeneza kiuchumi? Akazane mpaka wapi? Na tena, mbona wasiokazana sana kwa kipimo chetu, hawaonyeshi dalili za kupungukiwa zaidi?  Itoshe tu kusema   kuwa tunahitaji maarifa zaidi?  Maarifa hayo ndiyo nini? Au tena mbona wanaokazana zaidi hata kama pia wanatumia maarifa zaidi  hawawezi kujipa furaha ya kuridhika zaidi? Kwa hiyo lipo jambo jingine linalohusika na uboreshaji wa maisha ya uchumi kwa binadamu kuliko bidii, akili na nguvu zake.

  

Tuangalie jambo hili kwa njia ya mafundisho kutokana na mtaalamu fulani wa mahesabu. Kama  mfano tukimpa   Bwana Yesu, au Neno la Mungu au pia nafasi ya kumtafuta Mungu namba 1.  Hii ikiwa na maana ni jambo lililopo na linaendelea milele. Na mambo yaliyoko  ulimwenguni ambayo huchakaa na kutoweka tukayapa namba  0. Sasa wakawepo watu wawili na kila mmoja akaanza kwa njia tofauti. Wakwanza akaanza hivi:-

Anajali mwili wake ................0,  Anataka kula vizuri......................0,

Atajenga nyumba nzuri ............0,  Atakuwa na mali nyingi ...............0,

Ataoa au kuolewa ...................0,   Atakuwa na elimu nzuri ...............0,

Apate watoto  ........................0,   Awe na shamba zuri ..................0,

Na mengineyo ambayo anaweza kuyafikiria,  na halafu akakumbuka kwamba yeye ni mkristo hivyo anakwenda ibadani pia  ......1,     

Kwa huyu thamani yake itakuwa  ... 000000001.   Hivyo yote aliyonayo ni kama hayapo au hayana maana kabisa.

Lakini mwenzake aliyejua kwamba anapaswa kumtanguliza BWANA,  mwumbaji wa vyote akaanza kinyume cha hesabu hiyo hapo Juu.  Akaanza na BWANA YESU, 100000000 ...,  ameonekana kuwa na mafanikio makubwa ajabu.  Ukianza na Bwana Yesu kila unachojiongezea atakipa   maana kubwa.

 

Mtume Paulo anawaona watu kama huyo wa mfano wa kwanza hapo juu wasiokwenda kwa utaratibu.   2. Thes. 3: 6.  Utaratibu wa Mkristo ni kumtanguliza Mungu katika mambo yote.  Mungu anatazamia tumheshimu katika mambo yetu yote.

Bwana Yesu anaona kuwa yale ambayo mwanadamu anayohangaikia ni nyongeza ambayo Mungu atampa bila ya yeye kuhangaika hivyo kama mwanadamu ataelewa linalompasa, yaani kile kimfaacho hasa katika maisha yake.

 

 

 

 

MWISHO

Mwanafunzi wa Yesu alimwambia   "Bwana nipe ruhusa kwanza, niende nikamzike Baba yangu".  Mt. 8:21 - 22.  Yesu alimwambia,  "Nifuate, waache wafu wazike wafu wao".

Neno hili ni Gumu lakini haiwapasi watu wa Mungu kufuatisha namna  za watu wa dunia hii hasa pale ambapo utumishi wao kwa Kristo utaingiliana na madai na matakwa na taratibu za kidunia.

Basi wapendwa, Mtafuteni Mungu kama watoto wanaopendwa.  Mtafuteni  maadamu anapatikana, Mwiteni maadamu yu karibu.

 

AMEN

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 



Rev. Peter MREMI
Chuo cha Biblia Mwika,
S.L.P. 3050,
MOSHI.
E-Mail:

(zurück zum Seitenanfang)