Göttinger Predigten

Choose your language:
deutsch English español
português dansk

Startseite

Aktuelle Predigten

Archiv

Besondere Gelegenheiten

Suche

Links

Konzeption

Unsere Autoren weltweit

Kontakt
ISSN 2195-3171





Göttinger Predigten im Internet hg. von U. Nembach

7 TH SUNDAY BEFORE EASTER (GUINGUAGESIMA), 18.02.2007

Predigt zu MATHAYO 16:21-27, verfasst von Grayson Z. Mstango

Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu na Ushirika wa Roho Mtakatifu ukae nanyi nyote. Amen.

SOMO: INJILI YA MATHAYO 16:21-27

Sala: Karibu Yesu, useme nasi kwa Neno lako la uzima. Amen.
Kichwa: Tazama Tunapanda kwenda Yerusalemu :
Shabaha: Wasikilizaji, wakumbuke upendo wa Mungu kwa njia ya Kristo na wajitoe kumpenda na kuwatumikia wengine.

Utangulizi :
Katika maisha yetu ni muhimu kujiuliza maswlai haya: ?Ni kwa nini Yesu alikubali mateso na kifo cha aibu msalabani? Je, hapakuwa na njia nyingine inayofaa katika kuwakomboa wanadamu?

1. Msalaba ni Njia ya Wokovu :

* Mazingira ya somo yanaonyesha kuwa pamoja na kwamba wanafunzi wa Yesu walimwelewa kuwa ni Masihi wa Mungu, lakini hawakuelewa vizuri maana yake. Wao walimuelewa kama Mkombozi atakayetawala kwa nguvu na kuuondosha utawala wa Kirumi katika nchi na taifa lao la Kiyahudi.

* Hii ndio maana Yesu anachukua hatua ya kuwafungua macho na kusema imempasa kwenda Yerusalemu na huko atapata mateso mengi toka kwa wajumbe wa Baraza Kuu la Dini ya Kiyahudi (Sanhedrini) Wazee, Wakuu wa Makuhani na Waandishi na kuuawa, na siku ya tatu atafufuka.

* Petro asiyeelewa vizuri mpango wa wokovu kwa njia ya msalaba na maana yake, alichukua hatua kumkanusha Yesu, na kumwambia yale ayasemayo hayatatokea kwake. Msalaba ni tishio na hakuna mtu awaye yote anayetamani kifo cha uchungu.

Yesu akikumbuka majaribu yote ya shetani na hila yake ya kuzuia mapenzi ya Mungu, kuwaokoa wanadamu wenye dhambi (Luka 4:13), kwa upole alimkemea shetani aliyekuwa ndani ya Petro ? ?Nenda nyuma yangu shetani, u kikwazo kwangu, maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu? (mst. 23). Kwa maana nyingine Shetani huna mamlaka wala uwezo wa kuuzuia msalaba kuwa sababu ya wokovu kwa wenye dhambi. Shindwa sasa, toweka sasa!

* Yeyote anayetaka kuifuata njia hii ya msalaba, hana budi kujikana. Kujikana sio kufunga tu kwa kuacha mambo fulani fulani tunayoyapenda. Labda hii ni sehemu tu, lakini muhimu ni kusema mapenzi yangu hapana ila ya Mungu yatimie, Mungu ayatawale maisha yangu n.k. Kujitwika msalaba ni maisha ya kujitoa dhabihu. Yeyote anayetambua neema hii inampasa kuachana na ubinafsi na kujitoa kikamilifu kumtumikia Kristo. Kumfuata Yesu ni kujitahidi daima kumtii na kufuata hatua zake zote. Mawazo, maneno na matendo yetu yote yatoe ushuhuda kuwa tu wafuasi wa Kristo.

* Dunia na yote yaliyomo ndani yake ni mazuri, ila hayaleti wokovu. Mtu atayeyangangania na kuacha kumtegemea Mungu mwisho wake utavuna hasara.

* Ni sababu hii Yesu anatukumbusha juu ya utoaji wa hesabu siku ile ya Kristo. Tukijua haya, yatupasa daima kumtegemea Yesu kabisa na kujitoa kuwatumikia wengine, ili hatimaye tupate kuvuna baraka kuu, uzima wa milele.

2. Kuujali Wokovu :

* Mpaka hapa ni dhahiri kuwa kila mmoja anaiona wazi njia ya wokovu. Yesu aliyekubali kwenda Yerusalemu, kuteswa na kuuawa wakati ulipotimia, aliuawa na kumwaga damu yake ya thamani kwa ajili ya wokovu wetu. Tunapowaza juu ya haya, tunakumbuka upendo wa Mungu wa ajabu maishani mwetu wa kumtoa mwanawe wa pekee (Yoh. 3:16).

* Lakini kukumbuka tu hakutatusaidia! Wako wengi wanaokumbuka au kusikia juu ya yale yote yaliyompata Yesu Msalabani, lakini hawaujali wokovu huu. Je tutapataje kupona tusipojali wokovu mkuu namna hii. (Waebr. 2:3).

Ili kuthibitisha vile tunavyojali wokovu huu, hatuna budi kila mmoja wetu kujichunguza na kuona vile anavyojikana, kujitwika msalaba na kumfuata Kristo kila siku na katika maisha yake daima.

* Ukiona Yesu si Mtawala wa maisha yako, umeshindwa kuachana na tabia ya ubinafsi na kujitoa kumtumikia Kristo na wenzako; aidha umeshindwa kumtii Kristo, mawazo, maneno na matendo yako hayamshuhudii Kristo na unavutwa zaidi na tamaa za dunia hii; Neno la Mungu halina nafasi kwako, wala maombi, ni ushuhuda wa kutosha kuwa huujali wokovu mkuu wa Yesu.

3. Hitimisho :

* Msalaba ndio njia pekee ya wokovu na Mungu aliichagua kwa makusudi yake. Inawezekana wakatokea watu wengine wanaotangaza njia zao, lakini wokovu ni kwa njia ya Yesu tu kama tunavyoona katika Mdo. 4:12, ?Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo?.

* Kwa ujumbe wa Neno hili la Mungu, ikiwa hujapokea Neno la wokovu wa Yesu ni nafasi yako sasa. Kwa wale ambao walishampokea Yesu lakini maisha yao yanathibitisha kuwa wameshindwa kuujali wokovu huu, hii ni nafasi yao kujihoji (Zaburi 139:23-24), kutubu na kisha kuendelea kumwamini na kumtegemea Yesu na Msalaba wake ulio sababu ya wokovu wetu.

Mungu na atubariki sisi sote kwa Neno lake.

Sala: Bwana Yesu tunakuomba msalaba wako uwe sababu ya wokovu wa kila mmoja wetu. Amen.

Mhubiri: Mchg. Grayson Z. Mstango
Mwika Bible College ,
Box 3050 ,
Moshi

Mwika Bible College
E-Mail: mwika@elct.org

(zurück zum Seitenanfang)