Göttinger Predigten

Choose your language:
deutsch English español
português dansk

Startseite

Aktuelle Predigten

Archiv

Besondere Gelegenheiten

Suche

Links

Konzeption

Unsere Autoren weltweit

Kontakt
ISSN 2195-3171





Göttinger Predigten im Internet hg. von U. Nembach

SIKU YA BWANA YA 6 KABLA YA PASAKA (INVOCAVIT), 25.02.2007

Predigt zu Matthäus 4:1-11, verfasst von Israel Y. Natse

Utangulizi:

Kwa kawaida ili kuthibitisha ufahamu au uelewa juu ya jambo fulani au mafundisho fulani mhusika ni lazima apate kupimwa au kujaribiwa.  Ziko njia nyingi za kumpima au kumjaribu mhusika huyo.  Kwa mfano, kwa kumpa mtihani wa kuandika au wa mdomo.  Kusudi la mtihani au mitihani hiyo ni ili kufahamu kama kweli mhusika anaelewa vizuri hilo analopaswa kupimwa kwalo.  Hivyo kupimwa au kujaribiwa (tested) ni jambo la lazima.

  

Bwana Yesu anajaribiwa na Ibilisi Jangwani:

Mpendwa msomaji wangu, Mwinjilisti Mathayo anatueleza kuwa, Yesu mara tu baada ya kubatizwa/kupokea nguvu - Roho Mtakatifu alipandishwa nyikani kujaribiwa na Ibilisi.  Kama nilivyosema hapo awali, kwamba kujaribiwa maana yake ni kujithibitisha katika ufahamu au uelewa wako katika lile ambalo kwayo unapimwa au kujaribiwa (tested) iwe ni IMANI au katika masomo yako.  Ni kweli mtu hawezi kujaribiwa au kupimwa kwa jambo ambalo hajui au hakufundishwa.

 

Mpendwa msomaji wangu, Mwinjilisti Mathayo anatueleza kwamba Yesu alijaribiwa mara tu baada ya ubatizo wake na Roho Mtakatifu kumjilia (mst. 16).

 

(i)                  Jaribu la Chakula (Mst. 3-4)

Mpendwa msikilizaji wnagu, Yesu alipandishwa na Roho nyikani ili apate kujaribiwa na Ibilisi.  Yesu alifunga siku arobaini mchana na usiku bila kula, mwishoni akaona njaa.  Ndipo mjaribu akaona atumie nafasi hiyo kumjaribu kuona kama kweli Yesu atasimamia kweli yake.

 

Katika mstari wa tatu, Mjaribu anamtaka Yesu ageuze mawe yawe mkate ili apate kula maana ana njaa.  Jibu la Yesu ni kinyume kabisa na tegemeo la mjaribu; kwamba mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.  Yesu hakatai kuwa mkate ni muhimu kwa kuishi, ila kuna la muhimu zaidi hasa akiangalia zaidi nia na kusudi la mjaribu.

 

Mpendwa msomaji wangu, jaribu la chakula ni jaribu baya sana ambalo hukumba watu wengi sana katika kutetea/kusimamia Imani na hata maadili yao.  Wengi wameshindwa katika jaribu hili na hata kuuza uhuru wao na kufuata matakwa ya wale/yule anayetoa chakula.  Ukiangalia migogoro mingi inayotokea vyuoni/mashuleni na hata katika nchi nyingi masikini duniani ni kwa sababu ya kukosa chakula.  Hii ni kweli kwani chakula ni uhai, lakini Yesu anatukumbusha kuwa kuna cha zaidi ya chakula - Neno la Mungu - Chakula cha roho.  Yesu alishinda jaribu hili kwa kumtegemea Mungu - Baba yake.  Hivyo ni dhahiri kwamba mwanadamu kwa nguvu zake mwenyewe hawezi kushinda majaribu; bali kwa kumtegemea Yesu.

 

2

(ii)                Jaribu la Madaraka/Cheo/Kiburi (Mst. 5-6)

Mpendwa msomaji wangu, Ibilisi baada ya kushindwa katika jaribu la kwanza anamchukua Yesu na kumweka juu ya kinara cha Hekalu - anamwamuru kama kweli ndiwe mwana wa Mungu basi ajitupe chini maana imeandikwa atamwagizia malaika zake wamchukue.  Yesu anamjibu imeandikwa "Usimjaribu Bwana Mungu wako".  Mpendwa msomaji wangu, jaribu hili linawapata na kuwanasa wengi kwa kuonesha kiburi chao, vyeo vyao, ukuu na mamlaka yao.  Angalia jinsi Yesu alivyoonesha utii, unyenyekevu na hata kumpa Mungu sifa, heshima na utukufu.  Msomaji wangu, pengine kwa wengi ingekuwa nafasi yao kuonesha umaarufu wao, nguvu zao maana wanao ulinzi nyuma yao; kiburi cha uongozi, madaraka na kuondoa hekima, unyenyekevu utii na hata kuondoa hali ya kumtegemea na kumtumaini Mungu katika utendaji wao.

 

Msomaji wangu wiki hii tunaongozwa na neno kuu linalotuasa kwamba tukimtegemea Yesu tutashinda majaribu.

 

(iii)             Jaribu la Mali/Utajiri (Mst. 8-10):

Mpendwa msomaji wangu, Mwinjilisti Mathayo anatueleza juu ya Yesu kuoneshwa Milki na Fahari ya dunia hii na kutakiwa kumsujudia ili apewa.  Ndipo Yesu anapomjibu Ibilisi kwa ukali kabisa, "Nenda zako Shetani".  Kwani imeandikwa Msujudie Bwana Mungu yeye pekee yake.  Yesu alishinda jaribu hili kwa kumtegemea Mungu (Baba) yake.

 

Mpendwa msomaji wangu, jaribu la mali/utajiri na fahari ya dunia hii limekuwa jaribu baya sana linalowahangaisha watu wengi sana.

 

Watu wengi wamejiingiza katika mambo ya ushirikina/uchawi katika kujitafutia utajiri na mali.  Angalia matukio ya kafara zinazotolewa ili kupata mali/utajiri.  Matukio ya watoto wadogo kuuawa kwa kisingizio cha kutafuta mali.

 

Watu wengi wamejiingiza katika jaribu hili kwa kutafuta nguvu za giza/uchawi na kushindwa kumtegemea Yesu.  Mpendwa msomaji wangu, itaamfaa nini mtu kuupata ulimwengu wote na kuipoteza nafsi yake?  Utajiri/mali na fahari ya kweli ni kwa Yesu tu.

 

(iv)              Hitimisho:

Ni kweli msomaji wnagu, kwamba kwa kutegemea nguvu zetu wenyewe hatutaweza kushinda majaribu.  Jaribu la chakula, jaribu la vyeo/madaraka na kiburi cha uongozi pamoja na jaribu la mali/utajiri na fahari ya dunia hii yamewakumba wengi leo.  Na wengi wameshindwa katika majaribu hayo.  Mpendwa msomaji wangu, tutaweza kushinda majaribu haya kwa kumtegemea Yesu tu, maana yeye ni MSHINDI, nasi tutashinda hakika tukimtegemea.  "Nayaweza yote katika yeye anitiaye nguvu".  AMIN.

Israel Y. Natse
Mkuu wa Chuo,
Mwika Bible College

E-Mail: mwika@elct.org

(zurück zum Seitenanfang)