Göttinger Predigten

Choose your language:
deutsch English español
português dansk

Startseite

Aktuelle Predigten

Archiv

Besondere Gelegenheiten

Suche

Links

Konzeption

Unsere Autoren weltweit

Kontakt
ISSN 2195-3171





Göttinger Predigten im Internet hg. von U. Nembach

MAHUBIRI YA TAREHE, 04.03.2007

Predigt zu Lukas 7:36-50, verfasst von Mchungaji John Anderson Moshi

Utangulizi: Katika mazingira yetu ya sasa, mwanadamu amekuwa na tabia ya kukumbuka zaidi ubaya kuliko uzuri! Hata kama mazuri aliyoyaona ni mengi kuliko mabaya, yale mabaya yanapata nguvu kuliko yale mazuri, hii ni roho ya ajabu! Siwezi kuamini kwamba roho inatoka kwa Mungu. Ni rahisi kwangu kuamini kwamba roho ya aina hii inatoka kwa ibilisi.

 

 

Jumapili hii ningependa tuangalie mambo machache ambayo yatatuongoza katika neno la Mungu katika injili ya Luka.

 

 

Kwanza, kutambua dhambi yako ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Tunamwona mwanamke aliyetambua dhambi yake, akatafuta chupa ya marimari yenye marhamu, alisimama karibu na miguu yake. Huu ni utayari wa kutambua dhambi inayomtawala mtu. Kuna haja ya kweli ya mtu kila wakati kujiangalia na kujichambua kuhusu usafi wa moyo na usafi wa maisha ili kutambua endapo tuna dhambi ndani mwetu. Hata kama tuna kadhambi kama wengi wetu tunavyoweza kuweka dhambi kwenye ratili na kuona kuwa dhambi zingine ni ndogo sana na hivyo kujaribiwa kuona kuwa hakuna haja ya toba ya dhambi hizo. Mkristo anayetambua dhambi yake hata kama ni nyepesi sana, anaweza kuishi maisha ya toba na kuwa na mahusiano mazuri na Mungu. Kutambua dhambi ni kazi ya kujituma hasa wakati wa kujitafakari. Lakini kama hakuna tabia ya kujitafakari, si rahisi mtu kugundua kuwa ametenda dhambi hapa au pale. Maisha ya kujijua ni mazuri na yanafaa zaidi na hata wakati mwingine yanaleta amani na kumjenga mtu katika mwenendo mzima wa kiimani. Mtu wa aina hii anakuwa na mahusiano mema na Mungu na matumaini ya kwenda mbinguni ni makubwa.

 

 

Pili, kujutia dhambi ni ishara ya kuichukia na kuikataa. Tunaambiwa habari za mwanamke aliyesimama karibu na miguu ya Yesu akilia, na kuanza kudondosha machozi kwenye miguu ya Yesu na kisha kuipangusa kwa nywele zake. Inavyosemekana, mwanamke huyu alikuwa kahaba na mwenye dhambi. Farisayo aliyesema moyoni mwake kwamba hakutambua kwamba wenye dhambi ndio ambao Yesu anawatafuta, lakini kabla Yesu hajampata huyu, tayari mwenye dhambi amejuta na kumuendea Yesu ili amuondolee mzigo wa dhambi alionao. Hali hii inaonyesha kuwa mwanamke huyu amechukia dhambi zake zote na hataki tena kuendelea kutenda dhambi. Alionyesha hitaji la kweli la toba. Amejua kwa hakika kwamba Yesu pekee ndiye anayeweza kumsamehe dhambi zake. Kama mtu hajaweza kujutia dhambi zake atawezaje kuililia? Swala la unafiki hapa halipo kwani kinachotakiwa ni kuichukia dhambi, kama hilo halipo, inawezekana kabisa dhambi hiyo ikaendelea kutendekeka. Tabia ya kukataa dhambi ingalipo si tu kwa watu wanaoonyesha unafiki wa kutotaka kujua neema ya wokovu mahali ilipo bali wapo wanotubu na baada ya dakika chache kuirudia tena. Naweza kusema kuwa hii ni imani dhaifu sana katika mwenendo mzima wa mkristo.

 

 

Tatu, kutubu ni kutambua neema ya wokovu wetu ulioletwa na Yesu Kristo. Mungu alifanya hivi si kwa sababu sisi ni wema sana, la, bali kwa sababu hataki hata mtu mmoja apotee, bali apate uzima wa milele. Kwa mkristo kutotambua neema ya wokovu ni kukataa waziwazi kifo cha msalaba pale msalabani. Neema hapa si bure bali kwa kuwa ilitupasa sisi kufa kwa kuwa wadhambi sana na tusiofaa mbele za Mungu, inatubidi kutambua kwamba neema hii ilimgharimu damu yake ya thamani na mateso mengi na kudharauliwa kwingi kwa ajili ya dhambi tulizomtendea Mungu. Wapo watu wanaofikiri kwamba maana ya neema katika dhana hii ni bure!! Hasha si bure, bali kuna damu mahangaiko, dharau, mateso na damu kumwagika, hapa hatuwezi kusema ni itu cha bure, wala hatuwezi kusema kwa kuwa hatujateseka kama Yesu, bali wokovu umekuja kwetu bure. Hii ni dhana isiyofaa hasa kwa mkristo. Mkristo anapaswa aone uchungu juu ya tukio hili na alitazame kwa uchungu huo na kwa masononeko ya ndani ya imani yake liguse maisha yake na libadilishe mwenendo mbovu aliokuwa nao na kumrudisha kwa Yesu.wakati huu wa kwaresma ndio wakati unaofaa zaidi kuangalia na kutafakari juu ya kifo cha msalaba. Ndio wakati wa kusimama mbele ya Yesu Kristo kwa uchungu na majuto makubwa ukihitaji toba ya kweli pale ulipomkosea Mungu. Hata Mungu ataelewa kwamba wanangu wametambua neema ya wokovu wao. Mwaka huu si wa mara ya kwanza kwa wakristo kuiona kwaresma, wengine ni mara chache na wengine ni mara nyingi. Kuna kitu pia cha kujiuliza hapa, vipindi vyote vya kwaresma vimekusaidia kwa kiasi gain katika maisha yako ya imani? Umepiga hatua kwa kiasi gain? Umetubu kwa hakika au ni ili kipindi kikipita basi, tuanze maisha yaleyale ya zamani? Majira haya yanatukumbusha tu, bali hali nzima ya toba ni ya kila siku. Tusiposimama hivyo, tutajisahau na mwisho itakuwa ni utamaduni tu kuiona kwaresma!!

 

 

Nne,Watenda mabaya sana (dhambi nyingi) watasamehewa pia. Kwa Yesu, dhambi ni dhambi na hakuna nyingi na chache. Yule farisayo alisema moyoni mwake, Mtu huyu kama angekuwa nabii, angemtambua mwanamke huyu amgusaye, ni nani, naye ni wa namna gani, ya kwamba ni mwenye dhambi. Ndipo Yesu akitambua mawazo ya Farisayo huyo, alimjibu akimtaka amwambie ni yupi kati watu wawili wanaodaiwa, atampenda mdai wao atakapowasamehe, ni anayedaiwa dinari mia tano au ni anayedaiwa dinari hamsini. Yesu anasema kitendo cha mwanamke yule kuonyesha unyenyekevu mkubwa namna ile, amesamehewa dhambi zake ambazo ni nyingi. Farisayo hakuonyesha unyenyekevu wowote kwa Yesu Kristo kwani alijiona kuwa yeye ni mtenda dhambi kidogo ukilinganisha na yule mwananmke. Yesu anamalizia kwa kusema, asamehewaye dhambi nyingi, hupenda zaidi, na asamehewaye kidogo hupenda kidogo. Yesu alionyesha jinsi Farisayo huyo ambavyo hakujali dhambi yake ndogo kwamba isingemnyima kwenda katika uzima wa milele, hasa alipojilinganisha na mwamnamke yule.

 

 

Tano, tuache kuwanyooshea vidole wenye dhambi, kumbe sisi ...! Tabia ile ya kujiona kuwa mimi ni nafuu zaidi kuliko yule, inaponza wengi na kuwafanya wengine wasione haja ya kutubu. Farisayo akasema, angemtambua mwanamke huyu .... Lakini hakujikagua yeye mwenyewe jinsi alivyo, na ilikuwa ni vigumu sana kwake yeye kujitambua na dhambi alizo nazo. Waweza kuona fulani hafai katika jambo fulani kumbe wewe ungefanya vibaya zaidi kama ungepewa nafasi hiyo. Twaweza kukosoana sana tunapokuwa pamoja katika hata huduma, kwamba mimi naweza kuomba zaidi kuliko fulani, au kuimba zaidi kuliko fulani au kuhubiri zaidi kuliko fulani, kumbe wewe waweza usifanye vizuri kama yeye anavyofanya. Hata taifa moja laweza kuliona taifa lingine kwamba linawatendea watu wake vibaya na hivyo linastahili adhabu fulani, kumbe hata taifa lako lina jambo ambalo ni baya kuliko la taifa lile unalodhani kuwa ni baya. Wakristo wanaojitambua vizuri na wanaotunza ukristo wao vizuri, lazima waone unyonge wa ndugu zao kama wa kwao, na hivyo kuchukua jukumu la kuwaombea na kuwasaidia. Tukumbuke maneno ya Yesu Kristo kuwa, "mpende jirani yako kama nafsi yako". Kama kuna wema ambao Mungu amekutendea usione kwamba wema huo uliustahili sana au wewe ni mwema sana ndiyo maan Mungu amekuzawadia wema huo, bali utazame kama changamoto kwako na jinsi utakavyoushiriki wema huo na ndugu zako au jirani zako. Unavyopokea mengi kutoka kwa Mungu ndivyo utakavyodaiwa mengi. Jione kama mtu unayehitaji zaidi kusamehewa hata mbele ya wenye dhambi kuliko kuiona dhambi ya wengine na kwamba hawastahili kwenda mbele za uso wa Mungu hata kwa toba. Tukumbuke kwamba Mungu anataka hata mmoja asipotee bali awe na uzima wa milele. Tena Yesu asema, "...sikuja kwa ajili ya wenye haki bali kwa ajili ya wenye dhambi..." hivyo si sawa kuwahukumu wengine bali tunapowaona wanasogea mbele za uso wa Mungu tushangilie na kuwatia moyo ili iwe furaha kkubwa mbele za Mungu na ufalme wake wote. Tena iwe somo na kwetu sisi tuanofikiri tumekamilika sana ili tujitafakari hasa mienendo yetu ili tuone kama ipo hata siku moja ambayo tumekuja mbele za Mungu kwa toba au la. Tujenge tabia nzuri ya toba kila siku. Na majira haya yatufundishe hiyo tabia njema ya kila siku. Kama nilivyosema kama mtu hayuko karibu na Mungu au tuseme ametawaliwa na shetani, si rahisi kuomba msamaha hata kwa mume au mke wake, maana si tabia yake kufanya hivyo. Nni mtu wa kuwaona wengine kwamba hawafai na hawastahili tena ni wachafu.

 

 

Sita, imani kwa Yesu Kristo inaokoa na amani inatawala. Labda tupate kujiuliza swali moja sisi wakristo, tunajua ni wapi tunaweza kupata amani? Tunajua tusipopiga magoti miguuni kwa Yesu kwa imani hatutaweza kuokolewa? Yesu kristo alimwambia yule mwanamke, "Umesamehewa dhambi zako". Tena akamwambia tena yule mwanamke, "imani yako imekuokoa, enenda zako kwa amani". Nani asingependa kuambiwa maneno haya na Bwana Yesu Kristo? Hapana shaka kila mtu hasa mkristo angependa kuambiwa haya maneno. Ni maneno ya hakika na ya kutia moyo. Tunaona hata yule Farisayo pamoja na kumwona mwanamke yule kwamba ana dhambi, lakini, aliyetangaziwa wokovu ni yule mwanamke na wala sio yule Farisayo tena. Twaweza kufikiri kwa kuwaona wenzetu na uovu wao basi, nasi tutapata thawabu, kumbe ni tofauti kabisa. Yesu anatukumbusha juu kutambua hasa kazi aliyofanya na lengo la Mungu kumtuma kwetu.

 

 

Mwisho, neno linatufundisha tena kukumbuka neema za na rehema za Mungu kwetu ili tujue inavyotupasa kuenenda. Kipindi hiki cha kwaresma tukikumbuka vizuri wajibu wetu na maisha ambayo tunapaswa kuishi, tutaweza kuona dhambi zetu kuzijutia na kutubu kwa kweli ili tupokee msamaha na wokovu kutoka kwa Yesu Kristo mwenyewe.

Maisha ya kwaresma ni maisha ya toba na kurudisha mahusiano yetu sisi kwa sisi. Ni kipindi cha kujiangalia kwa upya na kuona mahali tulipomkosea Mungu ili tuweze kutengenza. Ni kipindi cha matengenezo ya kweli. Mwaka ungaliweza kuonekana kwako kuwa mwaka wa mapinduzi na mwaka wa kipekee katika maisha yako. Hebu kila mmoja aone hii ni kwaresma ya ngapi katika maisha yake, na unahitaji kwaresma ngapi ili utubu dhambi zako. Unahitaji kwaresma ngapi ili uone dhambi zako? Unahitaji kwaresma ngapi ili ujutie dhambi zako? Kama hayo yote hayajatendeka kwako, basi kipindi hiki fanya tofauti, onyesha majuto ya kweli ya ndani ya moyo wako, na uichukie dhambi kwa ukweli utakaoonekana na Yesu kristo, ili aone imani yako na akupokee kwa upya. Ujumbe huu kwa watu wote ambao wameamua kutengeneza maisha yao na kurejea kwa yesu Kristo kwa imani kwa kujutia dhambi zao na kutubu. Pengine usiwe na kwaresma nyingine kama hii, saa ya wokovu ni sasa. Amua sasa na yesu atakutangazia kama alivyomtangazia yule mwanamke aliyeonekana mwenye dhambi sana. Hata kama umefanya maovu mengi na yanaonekana kuwa ni mzigo usiosamahaka tena, Yesu atakusamahe, sio kama unavyofikiri.

 

Amani ya Mungu wetu itufunike sisi sote ili tupate kutambua siri hii aliyotungulia katika neno hili.

Mchungaji John Anderson Moshi

E-Mail: johnmoshi@yahoo.com

(zurück zum Seitenanfang)