Jude 1:17-23

Jude 1:17-23

TRINITY 18, OCTOBER 15, 2006
A Sermon Based on Jude 1:17-23 (UV) By Awumsuri Masuki


“ Bali ninyi,wapenzi,yakumbukeni maneno yaliyonenwa zamani na mitume wa Bwana wetu Yesu Kristo, ya kwamba waliwaambia ya kuwa,wakati wa mwisho watakuwako watu wenye kudhihaki, wakizifuata tama zao wenyewe za upotevu. Watu hao ndio waletao matengano, watu wa dunia hii tu, wasio na Roho. Bali ninyi, wapenzi,mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu sana, na kuomba katika Roho Mtakatifu,jilindeni katika upendo wa Mungu,huku mkingojea rehema ya Bwana wetu Yesu Kristo, hata mpate uzima wa milele. Wahurumieni wengine walio na shaka, na wangine waokoeni kwa kuwanyakua katika moto;na wengine wahurumieni kwa hofu,mkilichukia hata vazi lililotiwa uchafu na mwili.”

REHEMA, AMANI NA UPENDO WA KWELI HUPATIKANA KWA KUMWAMINI MUNGU.

Yuda ameandika waraka mfupi sana ila ni wenye ujumbe mzito kabisa kwa Kanisa. Kwanza yeye mwenyewe amekuwa mfano mzuri alipojishusha akijiita ‘mtumwa’ wa Yesu Kristo (mst. 1). Waandishi mbalimbali wamemwelezea Yuda kuwa ni ndugu waYesu ila yeye mwenyewe hakujitaja kama ndugu ila ni mtumwa. Kwa kujiita mtumwa anaonyesha jinsi alivyoandika kwa amri ya Yesu mwenyewe, maana mtumwa hawezi kufanya jambo bila kuamriwa na bwana wake.

Akiiwataja walioandikiwa, Yuda anawaweka katika kundi la watu waliopendwa na Mungu ambao wanahifadhiwa katika Yesu Kristo. Hawa walikabidhiwa imani ambayo imetolewa kwa watakatifu mara moja (yaani kwa kufufuka kwa Yesu mara moja hatakufa tena). Kwa maneno mengine, Yuda anataka wasomaji wake wakumbuke kwamba wamekabidhiwa imani na inawapasa kuilinda na kuing’ang’ania ili watu wasioikubali wasiweze kuwakosesha.

Katika mstari wa pili wa Waraka huu, Yuda ametaja mambo matatu ambayo ni ya msingi katika ujumbe wake wote alipoandika “ Mwongezewe rehema, na amani na upendano”. Neno mwongezewe linaonesha kuwa walikuwa navyo na sasa vimepungua au vimeondoshwa. Wokovu ulioletwa na Mungu kupitia Yesu Kristo ni kwa ajili ya watu wote. Maswali mbalimbali yaliyojitokeza kuonesha kuwa amani na upendo vimepungua na wanahitaji rehema ya Mungu. Je Mbona ndugu kwa ndugu wanagombana na upendo umepungua sana? Je mbona watu hawaaminiani tena kwamba zamani? Mbona imani kwa Mungu imepungua?

Katika maelezo yote ya waraka huu, inaonekana kuwa hayo yote yametokana na kudanganywa na watu wasioikubali kweli ya Mungu. Hivyo Yuda anawaandikia waamini akiwaonya na kuwakumbusha machache yahusuyo imani kwa Yesu Kristo ambaye ni kichwa cha kanisa.

1. Imani Kwa Mungu Huja na Kukua Tunapotafakari Neno Lake.

Neno la Mungu ni ushuhuda unaomulika mioyoni na kuonyesha njia ya ushindi pale

tunaposhindwa. Linafunua mambo mabaya yaliyofichika na kuyawaka wazi ili tuyaone na kuyaepuka. Pia neno la Mungu linashuhudia kweli kila siku na kila mahali.

Wanaolipinga neno la Mungu ni watu wasio na Roho wa Mungu. Watu hawa walitabiriwa tangu zamani kuwa watatokea siku za mwisho; ambao watadhihaki maneno yenye uzima, watafuata njia za upotevu na wataleta matengano duniani. Watu hao wameitwa ‘wa dunia hii tu’.

Neno la Mungu linamjenga anayelisoma naye huimarika katika Imani iliyo takatifu. Imani kwa Mungu Muumba anayetukomboa kwa njia ya Yesu Kristo na kututakasa kwa Roho wake mtakatifu. Neno la Mungu pamoja na kumjenga mtu, linamlinda pendoni mwake, linamwongoza ili apate rehema za Mungu na mwishowe linamwongoza mtu katika njia ya uzima wa milele.

2. Upendano hutoa matunda ya huruma

Upendo ni tunda la Roho. Mtu aliyejazwa na Roho wa Mungu atatoa matunda ambapo tunda mojawapo ni kupenda wengine. Biblia inasema kuwa asiyempenda ndugu yake ni sawa na muuaji- hamjui Mungu(1Yn.3:14-15). Mungu amejifunua kwetu kwa pendo lake la ajabu-Kumpenda mtu mdhambi. Anawataka watu wote wafuate upendo wake kwa kuwahurumia wengine. Wapo watu wengi wanaoangamia kwa kutofahamu au kwa kudanganywa na wenzao.

Ni wajibu wa kila aliyeuona upendo wa Mungu kuuonesha kwa wengine hata kwa kuwashurutisha ili waokoke na ghadhabu ya Mungu itakayowajilia waasi. Mtu yeyote ampendaye ndugu yake, ataonyesha upendo huo pale shida inapotokea.

Kumpenda na kumhurumia mtu haimaanishi kukubaliana na yale anayofanya bali huambatana na kuhuzunishwa na maovu yake na kuyachukia pamoja na kuchukua hatua itakayomwezesha kupata wokovu.

3. Mungu wetu ni wa rehema kwa wanadamu

Mawazo, maneno na matendo ya mtu siku zote yanaelekea kwenye upotevu. Hili linathibitika pale ambapo maovu yanapomtawala hata anashindwa kuyatenda mapenzi ya Mungu. Tatizo kubwa ni watu kutotambua na kujutia maovu. Yuda anawakumbusha watu wote kuwa waukubali upendo wa Mungu unaowavuta kwenye rehema yake.

Bwana wetu Yesu Kristo analipenda kanisa lake yaani watu wanaomwamini na analihurumia; amelifia msalabani na kwa kushinda kwake amelishindia. Wote watakaoliitia jina lake watapata rehema na kupata uzima wa milele.

Bwana wa kanisa anawaita watu wote na kuwataka wawe na upendano wa kweli-kumpenda Mungu na kupendana sisi kwa sisi na matunda ya upendo wetu yapate kuzaa matunda ya kuhurumiana. Pia tunaitwa kudumu katika neno la Mungu lililo dira ya Maisha ya ufuasi, linalotuonya na kutuongoza kwenye toba ili tupate rehema zake Mungu. Mwisho, tuyaepuke mabaya yote, tujivike upendo wa Mungu na tumtegemee Yesu Kristo aliye uzima wetu.

Bwana atubariki sote na atuwezeshe kumtegemea maisha yetu yote.


Rev. Awumsuri Masuki
Mwika Bible School
P.O. Box 3050
Moshi.
E-Mail: ajmasuki@yahoo.com

de_DEDeutsch