MATHAYO 24:35-44

MATHAYO 24:35-44

MAJILIO 2 NOVEMBA 19, 2006
MAHUBIRI NA MCH. ELIA M. MANDE KUTOKA MATHAYO 24:35-44


(Predigt in Kiswahili verfasst, aus Tansania)

Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo anasema, “Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kwamwe”. Ndivyo! Neno la Kristo ni la uhakika zaidi tena ladumu milele. Lakini tazama, mbingu na nchi zitapita. Hivyo yatupasa kujenga maisha yetu na matumaini yetu juu ya Neno la Kristo kuliko kujenga maisha yetu juu ya mbingu na misingi ya dunia hii, maana kuna wakati utakuja mbingu na nchi havitakuwepo tena. Lakini Neno la Kristo litakuwepo maana linadumu milele na milele.

HUKUMU YA MWISHO

Ndugu mpendwa, Kristo Yesu sasa analeta ujumbe huu maalum. Ujumbe kuhusu mbingu, kuhusu nchi na kuhusu wakati. Tazama wakati unakuja, wakati wa kutisha mno! Wakati unakuja wa hukumu ya mwisho. Hukumu ya mwisho wa dunia inakuja.

Nenda mahakamani wakati Jaji anapotoa hukumu kwa wafungwa waliofanya mauaji. Hukumu ya Jaji kwa waliofanya makosa hayo ya mauaji inatisha mno. Hukumu hiyo inapotolewa wakati mwingine mkosaji huanguka chini na kuzirai ama kuzimia. Ndugu na jamaa zake nao huchanganyikiwa na kuomboleza sana. Hukumu inatisha sana. Iwapo hukumu itolewayo na Jaji hapa duniani inatisha hivyo, sembuse ile hukumu ya mwisho wa dunia! Tena hiyo itatolewa na Bwana wa Mabwana. Hatuna maneno ya kueleza jinsi inavyotisha. Na ya kwamba mbingu na nchi zitatoweka wakati wake utakapowadia, hilo kweli linatisha mno. Kweli itakuwa ni siku ya maajabu. Maana kutakuwa na nchi mpya na mbingu mpya.

SIKU YA KUSHANGAZA

Siku ile ya kushangaza inakuja. Ni siku ya kustaajabisha. Na la kustaajabisha zaidi ni hili kwamba, hakuna aijuaye siku ile na saa ile. Neno la Mungu linasema, “Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana ila Baba peke yake.” Mt. 24:36.

Mpendwa katika Kristo, Neno la Mungu linaonya kwamba siku hiyo itakuja kama ilivyotokea nyakati za Nuhu. “Kwa kuwa kama vile siku zile zilizokuwa kabla ya Gharika, watu walivyokuwa wakila, na kunywa, wakioa na kuolewa, hata siku ile aliyoingia Nuhu katika safina, wasitambue, hata gharika ikaja, ikawachukua wote, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.” Mt. 24:38-39. Ni kweli wakati ule wa gharika dunia iliangamia. Nuhu tu na familia yake, jumla ya watu tisa tu, walipona. Wote wale walioangamia ni kwamba hawakuwa na habari kuhusu gharika. Walipewa ujumbe mapema. Lakini hawakuupokea ujumbe, walidharau tu. Hawakujali.

Ndivyo ilivyo pia katika ulimwengu wetu wa leo. Hukumu ya mwisho inakuja. Si wote watakaoupokea ujumbe huu mzito. Wengine wanaona miaka na miaka imepita, hili halijatokea. Hivyo, halipo. Halitakuwepo. Hawalipokei Neno hili kutoka kwa Bwana.

Watu wapo katika shughuli zao mbalimbali, watu wapo katika starehe na anasa za dunia hii. Wengi wanamsahau Mungu. Watu wanaoa na kuolewa, waakula na kunywa, tena wengine wanalewa chakari. Wengine wapo kwenye biashara zao, kwenye kazi zao. Wanatafuta mali na pesa kwa njia mbalimbali usiku na mchana. Ndiyo, ni sawa na nyakati za Nuhu. Wengi imani yao imepoa, wengi upendo wao kwa Bwana Mungu umepoa. Ujumbe huu unakuja kwa wakati wake.

Tazama jinsi itakavyokuwa siku hiyo ya hukumu ya mwisho. Watu wawili watakuwa pamoja, mmoja atwaliwa, mmoja aachwa. Wawili watakuwa wakifanya kazi pamoja, mmoja atwaliwa na mmoja aachwa. Wawili watakuwa safarini, mmoja atwaliwa na mwingine aachwa. Wanawake wawili wakisaga, mmoja atwaliwa, mmoja aachwa.

KESHENI

Ndugu mpendwa katika Bwana, Kristo Yesu anatuonya akisema, “Kesheni hasi, kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu.” Mt. 24:42. Itakuwa ghafla kama vile mwivi anavyovunja nyumba na kuiba.

Huo ndio ujumbe mkuu wa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo kwa watu wote. Ujumbe wake ni wa kweli na wa hakika. Katika Maandiko Matakatifu, yeye mwenyewe anasema akithibitisha kwamba kuja kwake hapa duniani ni kwa ajili ya hukumu, “Yesu akasema, Mimi nimekuja ulimwengunis humu kwa hukumu, ili wao wasioona waone, nao wanaoona wawe vipofu.” Yn. 9:39. Tusiwe kama wale Mafarisayo walivyoushangaa ujumbe huu, nao wakadai wanaona, kumbe ni vipofu na wakadumu dhambini pasipo kutubu.

Kisiwa kimoja katika bahari ya Atlantic, kilikuwa na mlima wenye volkano. Mlima ulipozidi kumwanga tope la moto wakaaji wa kisiwa hicho walionywa kukihama kisiwa hicho haraka kabla ya kuangamia. Wachache walifanya uamuzi wa busara. Waliingia melini na kwenye mashua wakahama. Wengine walidharau. Hawakujali maonyo. Lakini ghafla mlima ulitoa moshi mnene sana isivyokuwa kawaida yake. Tena ulimwaga tope la moto kwa wingi na kuenea kisiwa kizima. Watu wote na viumbe vyote viliangamia.

Ndugu mpendwa, nasi leo tunapewa wito wa kukesha. Tunapewa wito wa kujiweka tayari maana wakati wo wote Bwana atarudi mara ya pili duniani. Wakati wo wote hukumu ya mwisho inakuja. Dalili zake ni dhahiri. Tusije tukaangamia kama wale wakaaji wa kile kisiwa walioziba masikio yao na waliofanya shingo zao kuwa ngumu. Waliangamia, wewe wajua mahali ulipo. Sijui upo katika dhambi gani, Tuondoke mahali tulipo. Iwapo hapo mahali ulipo kuna dhamba inayokutesa na kukuhangalisha usiku na mchana, sasa ni wakati wa kuondoka kwani hapo ni mahali pa hatari kwa maisha yako ya sasa na yajayo. Ni wakati wa kutubu.

Tukeshe katika kuomba. Tujiweke tayari, kwa kuwa katika saa tusiyoijua, Mwana wa Adamu yuaja.

“Na Mungu wa Neema yote, aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele katika Kristo, mkiisha kuteswa kwa muda kidogo, yeye mwenyewe atawatengeneza, na kuwathibitisha, na kuwatia nguvu. Uweza una yeye hata milele na milele. Amin. (I Pet. 5:10-11).


Elia M. Mande,
Chuo cha Biblia na Theologia Mwika,
S.L.P. 3050,
Moshi – Tanzania
E-mail: mwika@elct.org

de_DEDeutsch